Sakata vyeti vya Makonda kortini

*Meya Ubungo ajitosa kutafuta ukweli kisheria
*Kumshitaki Sekretarieti ya Maadili na Tume

Mwandishi Wetu

Meya wa Manispaa ya Boniface Jacob
MEYA wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, amesema yuko katika hatua za mwisho kufungua kesi mahakamani dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa madai ya kughushi vyeti vya elimu na nyaraka zingine.

Kwa mujibu wa Jacob, kesi hiyo itajikita kwenye maeneo manne makuu ambayo ni; Mkuu huyo kujifanya Paul Makonda, kula kiapo kwa Rais kwa niaba ya Paul Makonda, kujitambulisha ukuu wa mkoa na kutumia nyaraka kwa jina la Paul Makonda ambazo si za jina lake wakati yeye ni Daud Albert Bashite.

Jacob alisema hayo alipozungumza na gazeti hili jana akibainisha kuwa pamoja na kufungua kesi hiyo, pia atamshitaki Makonda kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).

Meya alisema wakili wa kesi hiyo atakuwa Peter Kibatala na wanasheria wengine wengi aliosema wamejitolea kusaidia ili ukweli ujulikane. Alisema hafanyi hilo kwa nia ya kumkomoa Makonda, bali kutaka kuhakikisha haki inatendeka kama ilivyotokea kwa watu wengine.

“Kuanzia Jumatatu, natarajia kufungua kesi mahakamani ambayo itamhusu Makonda kwa tuhuma za kughushi vyeti na kufanya kazi kwa jina lisilo lake,” alisema. Alisema atafuata taratibu zote muhimu kabla ya kufungua kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Alisema kitendo cha mtu kutengeneza nyaraka kwa jina ambalo lisilo lake ni kosa la jinai ambao haliwezi kuvumiliwa. Aidha, alisema Sekretarieti na Tume, anaamini kuwa ni vyombo vyenye mamlaka kwa watumishi wa umma.

Sakata la Makonda kudaiwa kughushi vyeti liliibuka katika mitandao ya kijamii takriban mwezi mmoja uliopita na kila alipoulizwa amekuwa akishindwa kulizungumzia hata wakati mwingine kutoa lugha chafu kwa waandishi wa habari.

Baadhi ya waandishi ambao walikumbwa na lugha chafu za Mkuu huyo wa Mkoa ni Mhariri wa Habari wa Gazeti hili, Exuperius Kachenje na mwandishi wa Tanzania Daima, Ibrahim Yamola.

Gazeti la JAMBO LEO lilikuwa la kwanza kuandika habari kuhusu elimu ya Makonda baada ya taarifa za mtandaoni kabla ya vyombo vingine vya habari hasa magazeti na mitandao ya kijamii, kuendelea kufuatilia huku Askofu wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat Gwajima akijitokeza na kudai kuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu kiongozi huyo kughushi vyeti.

Wamshangaa
Akizungumzia kitendo cha Makonda kusafiri nje ya nchi safari zisizo na tija, licha ya katazo la Rais John Magufuli, mkazi wa Dar es Salaam, Joel Nkwale alisema ni jambo la kushangaza kwa kiongozi huyo kusafiri wakati Rais yuko nchini.

“Kama sijakosea mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyapinga ni matumizi mabaya ya fedha za umma na Makonda amesafiri Marekani, Ufaransa na Afrika Kusini, sijui anatumia fedha za nani mbona hili halisemwi?” Alihoji Nkwale.

Joyce Temba wa Mwananyamala, alihoji Mkuu wa Mkoa alikopata fedha za kufanyia sherehe za mwaka mmoja na kurusha matangazo ya mbashara kwa zaidi ya saa tatu kwenye vituo tofauti vya televisheni, licha ya Rais kukataza matangazo mbashara kwa Bunge.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo