Wanahabari wapongezwa kumsusa Makonda


Suleiman Msuya

Paul Makonda
UAMUZI wa vyombo vya habari kumsusia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya naye kazi kumepongezwa na wadau.

Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati tofauti jana, wadau wa habari nchini walisema uamuzi huo umechelewa na kushauri kuwa ungehusu Serikali nzima kwa wanachodai kuwa anapewa kiburi na wakubwa zake.

Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari,

Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema kwa mtazamo wake anapongeza hatua hiyo, huku akisisitiza kuwa ingekuwa vema kutofanya kazi na Serikali nzima.

Sugu alisema kwa welewa wa kawaida inaonesha dhahiri anachofanya Makonda ni maagizo ya wakubwa wake wa kazi hivyo hakuna sababu ya kufanya kazi nao wote.

“Makonda ni sawa kutoandikwa ila naamini anachofanya si kwa uamuziwake, kuna watu wanamtuma ambao ndio wamempa nafasi hiyo inapaswa nao wasiandikwe,” alisema.

Mbunge huyo alisema haiwezekani Makonda kuchukua askari wote aliokwenda nao katika televisheni ya Clouds Media bila mkuu wake kuhusika, hivyo itakuwa vema nao kutoandikwa.

Alisema katika ulimwengu huu wa sasa ambao demokrasia inatakiwa kutamalaki, haingii akilini kuona tukio kama alilofanya Makonda likichekewa kwani linaweza kusababisha jamii kupotoka.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema uamuzi huo ni wakuungwa mkono na watu huo ili kuhakikisha kuwa mamlaka husika zikichukua hatua.

Dk Bisimba alisema pia angependa kuona zikiwepo hatua nyingine za kisheria kama kwenda mahakamani ili kuhakikisha kuwa haki inatamalaki nchini kwa watu wote.

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema uamuzi wa vyombo vya habari ungepaswa kufanyika tangu kupitishwa Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari ambayo ililalamikiwa na jamii nzima.

Alisema anachofanya Makonda ni kosa kisheria na hakiwezi kuvumiliwa na mtu yeyote na kwamba kila kona inalalamika kwa Serikali kushindwa kusimamia haki.

“Vyombo vya habari vimechelewa sana kuchukua uamuzi huu kwani wangepaswa kufanya hivyo katika mchakato wa sheria yenu ambayo imepitishwa hivi karibuni,” alisema.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu CCM, Daniel Zenda alisema haungi mkono uamuzi wa vyombo vya habari kutoandika habari za kikazi zinazomhusu Makonda na kwamba anaamini kuwa ni kutowatendea haki wananchi.

Alisema ni vema uamuzi huo ukawa ni kuzuia habari zake binafsi ili wananchi waweze kujua nini kinachoendelea katika mkoa huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo