Clouds ‘yamvua nguo’ Makonda


*Yasimulia jinsi alivyoivamia akiwa na askari
*Wamtaka aombe radhi ili kurejesha urafiki

Abraham Ntambara

Paul Makonda
MKURUGENZI wa Vipindi na Uendeshaji wa Kituo cha Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba, amethibitisha kituo hicho kuvamiwa na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda.

Ruge amesema baada ya kuvamia kituo hicho, mkuu wa mkoa alihoji sababu za kutorushwa hewani kipande cha video kinachoonesha mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kisha kutelekezwa.

Kauli hiyo ya CMG inaweza kuelezwa kuwa sawa na ‘kumvua nguo’ kiongozi huyo aliyejipatia umaarufu siku za karibuni kutokana na madai ya kutumia majina na cheti cha kidato cha nne cha mtu mwingine, huku mwenyewe akipata kigugumizi kulizungumzia hilo na badala yake kushambulia wanahabari.

Makonda alianza vituko kuhusu utata wa vyeti vyake Februari 21 alipotumia simu ya mwandishi wa gazeti hili, Salha Mohammed aliyeomba itumike kumpigia mhariri wake wa habari, Exuperius Kachenje, lakini badala ya kujibu maswali kuhusu vyeti vyake, mkuu huyo wa mkoa aliporomosha kashfa na matusi.

Siku iliyofuata, JAMBO LEO liliripoti kilichotokea na utata wa elimu ya Makonda, kabla ya vyombo vingine vya habari ambapo pia Mchungaji Gwajima alilizungumzia. Kabla ya jana, Askofu Gwajima amekuwa akimchambua Makonda kuhusu vyeti vyake, hata kufikia hatua iliyodaiwa kufanywa na kiongozi huyo kulazimisha kipindi cha kumchafua kiongozi huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Lakini jana, akizungumza kupitia Kipindi cha 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Ruge alisema pia video ya CCTV ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ikimwonesha Mkuu wa Mkoa akiingia kwenye studio zao na askari wenye bunduki kuwa imetoka kwao, lakini hajui aliyeisambaza.

“Video ya CCTV ni ya kweli na imetoka kwetu, lakini sijui nani aliitoa maana control room (chumba cha udhibiti) haiku mahali pa siri, watu wengi wanaweza kuaccess (kuingia),” alisema Ruge.

Alisema siku ya tukio – Ijumaa iliyopita - alipigiwa simu na mmoja wa wafanyakazi wake saa 5 usiku na kuarifiwa kuwa Makonda ameingia ofisini hapo akiwa na askari wenye silaha.

Ruge alisema tangu tukio hilo litokee alitarajia kuwa Makonda angeomba msamaha kwa kitendo chake kwa kurudi nyuma na kuonesha kukosea, lakini hadi jana hakuwa amefanya hivyo.

Alikiri kuwa Mkuu huyo amekuwa rafiki yao kabla hata hajawa mkuu wa mkoa wala wilaya ambapo alieleza kuwa pamoja na urafiki wao uliopo hahitaji urafiki wa bunduki.

Nape
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema kitendo hicho cha uvamizi unaodaiwa kufanywa na Makonda akiwa na askari ni tukio la kupingwa.

Aidha, alisema vitendo hivyo ni sawa na kunajisi uhuru wa habari ambapo alieleza kuwa kama yeye atashindwa kusimamia hilo hatafaa kuwa katika nafasi aliyonayo ya uwaziri.

Alisema kutokana na hali hiyo, kabla ya kuchukua hatua, kama Serikali watamsikiliza kwanza Mkuu huyo ambapo alieleza kuwa wameunda timu ya watu watano kufanya kazi ndani ya saa 24 ili wapate maelezo ya Makonda na kisha kutoa taarifa.

“Ripoti itakayotolewa na Kamati ya Uchunguzi pamoja na hatua zitakazochukuliwa vitatangazwa hadharani baada ya saa hizo 24,” alisema Nape.

Mengi
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Dk Reginald Mengi alimtaka Makonda kuomba radhi na asirudie kufanya kitendo cha namna hiyo.

“Jambo lililofanyika ni la hatari sana, lazima tujiulize mtu huyu (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam) anapata wapi ujasiri huu? Kama alikuja na bunduki hapa anaweza kwenda nazo popote na pengine kuna siku atazitumia,” alihadharisha Dk Mengi.

Alifafanua kuwa wanatambua kwamba Rais John Magufuli anapenda wanahabari ambapo aliutaka upendo huo usiwe wa maneno bali wa vitendo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CMG, Joseph Kusaga alimpa Makonda masharti ya kuomba radhi ili uhusiano wao uendelee kuwa mzuri.

Habari zaidi zilieleza kuwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na MOAT wako mbioni kutoa tamko kuhusu tukio hilo huku wakisubiri matokeo ya Kamati ya Nape.

Taarifa zingine zilipasha kuwa huenda Makonda akasusiwa ili taarifa zake zisitoke kwenye vyombo vya habari kama sehemu ya hatua ya kupinga kitendo alichokifanya dhidi ya CMG.

JPM
Hata hivyo wakati akihutubia kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma jana Dar es Salaam, Rais Magufuli alimtaka Makonda aendelee kuchapa kazi.

Rais Magufuli aliwataka Watanzania kuacha kisikiliza taarifa alizoziita za udaku kwenye mitandao ya kijamii na badala yake wajadili maendeleo.

Kauli ya Rais ilikuja wakati uvamizi huo dhidi ya CMG ukihusisha zaidi waandaaji wa kipindi cha De Weekend Chat Show maarufu kama SHILAWADU ambacho ni cha udaku na alichopata kukisifia huku akisema anapenda sana kukiangalia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba alisema alichofanya Makonda ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo hayajawahi kutokea tangu uhuru.

“Kwa namna yoyote, lazima tukubali kilichofanywa na Makonda ni matumizi mabaya ya madaraka. Tangu tupate Uhuru hakuna Mkuu wa Mkoa aliyewahi kufanya kitendo cha namna hii,” alisema Serukamba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo