Zanzibar yaruka kihunzi cha JPM


Fidelis Butahe

Dk. Shein na Dk. Magufuli Ikulu Dar es Salaam
SIKU 15 baada ya Rais John Magufuli kuliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia umeme wadaiwa wote ili wapate fedha za kuendesha shirika hilo kwa maendeleo ya Taifa, ikiwamo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayodaiwa Sh. bilioni 121, hatimaye Serikali hiyo imeanza kulipa deni.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Machi 6 mwaka huu wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha kupoza umeme cha njia ya Kv 132 mkoani Mtwara.

Siku tatu baada ya kauli hiyo ya Rais, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka alitoa siku 14 kwa Zeco, wizara na taasisi za Serikali kulipa madeni hayo kabla ya kukatiwa huduma.

Lakini jana, wakati ikiwa zimebaki siku nne kabla Tanesco haijaanza utekelezaji wa operesheni hiyo, Ikulu ilitoa taarifa ikieleza jinsi Rais Magufuli alivyokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na maofisa waandamizi wa Tanesco walioongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye aliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa hawatakatiwa umeme.

“Waziri wa Nishati na Madini amewatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa hawatakatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanza kulipa deni inalodaiwa na Tanesco,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ikimnukuu Profesa Muhongo.

“Tayari SMZ imeanza kulipa kiasi cha Sh bilioni 10 na itaendelea kulipa deni hilo mpaka litakapomalizika.”

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Profesa Muhongo alitoa wito kwa wadaiwa wote wa Tanesco kulipa madeni yao katika kipindi cha siku tano (mpaka kufikia jana) zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme.

Baada ya Tanesco kutoa siku 14, Dk Shein alizungumza na waandishi wa habari alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume, akitokea nchini Indonesia katika mkutano maalumu ulikomwakilisha Rais Magufuli na kusema kama nishati hiyo ikikatwa, watatumia vibatari kupata mwanga.

“Naamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Serikali ya kiungwana, inayojali watu wake, hivyo haiwezi kufanya hivyo kwenye suala hili la kuzima umeme visiwani Zanzibar na iwapo ikitokea umezimwa, Zanzibar watakuwa tayari kurudi kwenye matumizi ya vibatari,” alisema Dk Shein.

Katika maelezo yake ya Machi 9, Dk. Mwinuka alisema kitendo cha Tanesco kudai kiasi kikubwa cha fedha kunachangia kurudisha nyuma utendaji wa shirika hilo katika kusambaza huduma ya umeme nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo, baada ya muda waliotoa kwisha bila deni hilo kulipwa, Tanesco itachukua uamuzi mgumu wa kuwakatia umeme wadaiwa hao.

Alibainisha kuwa katika deni hilo, Zeco inadaiwa Sh bilioni 127, mashirika ya Serikali, wizara na taasisi Sh bilioni 52, huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa Sh bilioni 94.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo