Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar ataka ushirikiano


Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
 
Dk Shein

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Juma Abadallah Sadallah ‘Mabodi’, amewataka watendaji wa chama hicho kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha azma ya mageuzi yaliyofanywa ndani ya chama hicho hivi karibuni.

Akizungumza na watendaji hao baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi tangu ateuliwe kushika wadhifa huo wiki iliyopita, alisema viongozi wanapaswa kuwa sehemu ya mageuzi hayo ili kuleta tija kwa wananchi wote.

Sadallah ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika serikali ya awamu ya nne, alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha umoja na maelewano miongoni mwa jamii licha ya kuwepo kwa tofauti za kiitikadi.

Aliwataka kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015 hadi 2020 unaofanywa na serikali zote mbili ili kuwaondolea wananchi kero zinazowakabili na kwamba, hatamvumilia kiongozi au mtendaji atakayeshindwa kutekeleza maelekezo yanayotolewa na chama na serikali.

“Naomba tuendelee kushirikiana katika maandalizi ya uchaguzi wa dola wa mwaka 2020 kwa kuzisimamia serikali zitekeleze ilani ya uchaguzi ya chama chetu na tutakapoona kasi hairidhishi tutatekeleza kwa kutumia rasilimali za chama ilimradi wananchi wetu wasipate tabu,” alisema Mabodi.

Akizungumzia mikakati ya kukiimarisha chama, Naibu huyo alieleza kuwa, mbali ya kutumia nyenzo mbalimbali alizokabidhiwa na mtangulizi wake, Vuai Ali Vuai, alisema atatumia busara na hekima ili kuhakikisha chama hicho kinaongeza wanachama wanaokiunga mkono.

“Mtaji wa chama siku zote ni wanachama, jukumu langu na lenu kuhakikisha tunatumia mbinu mbalimbali za kuongeza wanachama na hatutaweza kufanya hivyo kama hatutawafuata mahali walipo,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Rahaleo, Unguja.

Akizungumzia namna atakavyosaidia kukuza ajira kwa vijana, alieleza kuwa mbali ya kusimamiwa kwa utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali na serikali, CCM itaanzisha na kuviendeleza vyuo vya amali ili kuongeza idadi ya watu wanaojiajiri.

Alisema mbali ya hatua hiyo kusaidia kupunguza tatizo la ajira, pia itasaidia kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali watakaotumika katika viwanda vitakavyoanzishwa nchini kutokana na utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda inayotekelezwa na serikali zote mbili za Tanzania.

“Hatuwezi kuingia katika uchumi wa viwanda bila ya kuwa na wataalamu wenye ujuzi mzuri, pamoja na serikali kutekeleza mikakati ya kukuza uchumi na chama kitafanya hivyo, si kwa lengo la kupunguza ajira tu, bali kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na tabia ya kuwa omba omba,” alisema Mabodi.

Akizungumzia hali ya amani na utulivu nchini, alisema atakuwa mstari wa mbele kuilinda Amani iliyopo na hatasita kukaa na mtu au kikundi chochote ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumu nchini.

“Nitatumia nguvu na uzoefu wangu wote kuhakikisha nchi inabaki salama hata kwa kuzungumza na watu ambao watakuwa wanaonekana kuwa na nia ya kuvuruga amani ya nchi yetu.

Hili nitalifanya kwa manufaa ya watu wetu ambao ndiyo waathirika wakubwa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo