Chirwa abeba jahazi la Yanga Zambia


Charity James

Obrey Chirwa
KASUSIWA timu! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa wale wapinzani wa timu ya Yanga mara baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa (pichani), kuwa ndiye mshambuliaji pekee katika kikosi cha timu hiyo kilichoondoka kwenda kurudiana na Zanaco.

Yanga inatarajia kuwa mgeni wa Zanaco ya Zambia katika mchezo wa marudiono wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo, Yanga itawakosa washambuliaji wao wawili tegemeo, Donald Ngoma na Amisi Tambwe ambao wanasumbuliwa na matatizo ya goti huku nafasi hiyo ikisalia kuwa mzigo kwa Chirwa ambaye ndiye atakayeongoza jahazi hilo ugenini.

Endapo Yanga ikipata matokeo mazuri katika mchezo huo, itakuwa imekata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Msaidizi wa klabu hiyo, Juma Mwambusi alisema bado hawajakata tamaa kuelekea mchezo huo pamoja na kukabiliwa na majeruhi wengi kwani wanaamini wana nafasi ya kufanya vizuri.

‘’Yanga inawachezaji wengi na mifumo huwa inabadilika, hivyo hatuna sababu ya kukata tamaa kwasababu ya kukosa wachezaji wawili katika kikosi tuna imani tutafanya vizuri na kuendelea katika hatua nyingine bila ya wachezaji hao,’’ alisema.

Alisema Ngoma na Tambwe ni wachezaji wazuri na wana umuhimu katika kikosi lakini kukosekana kwao haina maana kuwa watashindwa kufanya vizuri katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao kuhakikisha wanafanya vizuri ili waweze kuendelea katika hatua nyingine.

Mbali na wachezaji hao, wengine watakaokosa mchezo huo ni mshambuliaji Matheo Anthony, Ben Kakolanya, Pato Ngonyani, Malimi Busungu na Yusuph Mlilo.

Yanga haina budi kupata ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ndipo ikate tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo na endapo itatolewa itaangukia katika Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa mwaka jana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo