Quality Group yamuunga mkono JPM


Suleiman Msuya

CEO QGL, Nicholas Ralph
KAMPUNI ya Quality Group Limited (QGL), inaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizoko barabara ya Nyerere, Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL, Nicholas Ralph alisema katika kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi kampuni imeanzisha mfumo unaotambua na kudhibiti uhalifu huo kwenye taasisi (e-Governance).

Alisema mfumo huo wa utambuzi na udhibiti unapaswa kuwepo katika idara zote za Serikali, kwani una tija na ni salama zaidi hasa katika kuelekea katika Tanzania ya maendeleo endelevu.

Ralph alisema QGL imewekeza katika sekta mbalimbali kama afya ambapo wanatarajia kujenga vituo 4,000 vya afya nchini pamoja na vibanda vya kutoa afya ili kuendana na teknolojia ya sasa na kurahisisha kila mwananchi anapata huduma bora ya afya.

Alisema pia wamekubaliana na kampuni kutoka Urusi ili kusambaza vifaatiba na kampuni nyingine kutoka Marekani itatoa huduma ya ndege kwa huduma za dharura.

“Pia kampuni ya QGL imeingia makubaliano na kampuni ya Ireland kujenga na kusimamia viwanja vya ndege na kusaidia mafunzo ya teknolojia ya huduma za viwanja hivyo na hifadhi ya mafuta ya ndege,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL, alisema kampuni ya QGL imekuwa ikisadia wavuvi wa Kanda ya Ziwa kwa kuwapa vitendea kazi na matibabu, kusaidia elimu na pia ilisaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa Afrika.

Alisema kampuni hiyo imefanikiwa kuongeza ajira, mafunzo, kukuza uchumi ili kuhakikisha inaunga mkono mpango wa maendeleo wa Serikali wa Mwaka 2025.

Ralph alisema kampuni imekuwa ikitoa mafunzo kwa viongozi na waajiriwa vijana kupitia programu ya Moreh Derech ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa.

Aidha, alisema katika kuhakikisha inapanua ushirikiano na taasisi za kimataifa, imesaini makubaliano na kampuni ya Solanika International Tractors Limited ya India ambayo itakuwa inaingiza nchini matrekta 1,000 kwa mwaka, hivyo kuongeza ajira 1,200 ifikapo mwakani.

Hali kadhalika alisema wamewekeza katika viwanda vya sukari na maziwa ambapo wananchi wengi wa kitanzania ndio watafaidika kwa kuuza bidhaa husika katika viwanda hivyo venye teknolojia ya kisasa na uongozi kutoka Israel, Ulaya na Afrika Kusini.

Ralph alisema QGL imekuwepo kwa zaidi ya miaka 30 ambapo inashirikiana na kampuni kubwa duniani kama General Motors (GM), Honda, Isuzu, Bridgestone na Chevrolet.

Alisema kutokana na ushirikiano huo, QGL imeajiri zaidi ya wafanyakazi 667,300 na kupata faida ya dola za Marekani bilioni 348.6 hayo yakichangiwa na uwajibikaji, uwazi na uaminifu.
Alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanakuwa sehemu sahihi ya kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi wa Tanzania.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo