Yanga hakuna kulala


Asha Kigundula

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Klabu ya Yanga, wameamua kutolala kwa kuendelea na mazoezi ikionesha inataka kutetea ubingwa wake na kufanya vizuri katika michezo ya Ligi, Kombe la Shirikisho (FA)na kimataifa dhidi ya MC Alger ya Algeria mwezi ujao.

Katika mbio za kutetea Yanga itacheza mchezo wa kiporo dhidi ya Azam FC, utakaofanyika Aprili mosi mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Pia itakuwa ikijifua kwa ajili michezo mingine ya ligi na wa Kombe la Shirikisho dhidi ya MC Alger utakaofanyika Dar es Salaam kati ya Aprili 7 na 9 kabla ya kurudiana wikiendi inayoangukia Aprili 14 na16, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alisema wachezaji waliosalia kwenye kikosi baada ya wengine kuitwa katika timu ya taifa na wengine majeruhi wameanza mazoezi juzi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi uliopo Kurasini, Dar es Salaam.

Mkwasa alisema licha ya kuanza mazoezi hayo, kambi ya timu hiyo itaanza wiki ijayo baada ya kumalizika kwa mchezo kimataifa wa kirafiki wa timu ya Taifa, Taifa Stars dhidi ya Botswana, wachezaji walio katika timu hiyo wataungana na wenzao.

Kikosi cha Yanga kina wachezaji watano Taifa Stars ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Vicent Andrew na Simon Msuva.

Hata hivyo alisema washambuliaji Amissi Tambwe na Donald Ngoma, hawajaungana na wenzao katika mazoezi yanayoendelea kutokana na umajeruhi. Mkwasa alisema hana taarifa za maendeleo ya wachezaji hao, lakini kuna taarifa kutoka katika benchi la ufundi kuwa hawatacheza mchezo huo dhidi ya Azam FC.

“Tambwe na Ngoma bado majeruhi hawatacheza mchezo huo dhidi ya Azam kwa sababu wanaendelea na matibabu, watakuwa nje kwa muda wa wiki 10 kwa kuwa hawajapata nafuu ya kufanya waweze kuanza mazoezi na kuungana na wenzao,” kilisema chanzo jana.

Wawili hao, wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu, Tambwe ameumia goti na Ngoma ameshitua kifundo cha mguu baada ya kuumia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, visiwani Zanzibar.

Yanga inakabiliwa na mchezo huo mgumu wa ligi dhidi ya Azam FC ambao matokeo yake yatatoa sura ya kuendelea kupigania ubingwa wao walioupata uliopita, kwa sawa wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 53, wakizidiwa na watani wao wa jadi Simba alama mbili.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo