Mkuu wa majeshi: Kulikatia umeme jeshi ni kuhatarisha usalama wa nchi


Suleiman Msuya

Jenerali Venance Mabeyo (katikati) akizungumza
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo amesema suala la ulinzi halina mbadala na kwamba kusitisha huduma yoyote kwa jeshi hilo ikiwemo umeme ni kuhatarisha usalama wa nchi.

Mabeyo ametoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Upanga Dar es Salaam kuhusu deni wanalodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo ni zaidi ya Sh. bilioni 3.

Mkuu huyo wa majeshi alikiri kuwa wanadaiwa fedha hizo na Tanesco na kwamba leo watalipa Sh. bilioni moja ili kupunguza dani hilo.

“Tanesco itambue kuwa jeshi ni chombo muhimu kwa Taifa na kwamba kukikatia umeme ni kuhatarisha usalama wa nchi,” alisema Jenerali Mabeyo na kuongeza:

“Deni hilo linatokana na ufinyu wa bajeti jambo ambalo tunajipanga kukabiliana nalo.”

Alisema deni hilo linahusu vikosi vyake mbalimbali vinavyotumika katika uzalishaji, ulinzi na utawala hivyo Tanesco haina sababu ya kukimbilia kukata umeme kwani shughuli nyingi zitasimama.

“Nawaomba watuvumilie, lakini pia watambue kuwa kukata umeme katika ni hatari kwa nchi,” alisisitiza.

Alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa deni hilo linaisha huku akibainisha mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato katika jeshi hilo kupitia Kikosi cha Nyumbu, Suma JKT na Mzinga.

Ulipaji wa deni hilo unakuja takribani wiki mbili baada ya Tanesco kutoa wiki mbili zilizoisha jana kuwa litakata umeme kwenye taasisi za Serikali na sekta binafsi ambazo zimekuwa wadaiwa sugu ambapo JWTZ ni moja wapo.

Taasisi nyingine ilikuwa ni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambapo ilikuwa inadaiwa zaidi ya bilioni 121 na Tanesco na hivi karibuni ilipunguza deni hilo kwa kutoa Sh. bilioni 10.

Mabeyo alisema vikosi hivyo vitaboreshwa ili kuongeza uzalishaji ikiwa ni kutekeleza lengo la Rais kufikia uchumi wa viwanda.

Jenerali huyo alisema kwa kuanzia wameandaa waraka kwa Serikali ili ujadiliwe na Baraza la Mawaziri kuhusu Shirika Nyumbu kuboreshwa.

Mabeyo alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa mashirika hayo yanazailisha bidhaa ambazo zinatokana na malighafi za Kitanzania.

Alisema matumizi katika jeshi hilo yanaongezeka kutokana na ukubwa wake na mabadiliko ya teknolojia, hivyo ni vema wakawa na vyanzo vyao vya mapato ili kukidhi mahitaji yao.

“Jeshini kuna mitambo mikubwa ambayo inalinda nchi lakini pia inazalisha, tekonolijia imekuwa hali ambayo inachangia ongezeko la matumizi ya umeme hivyo vikosi vyetu vikijipanga kuzalisha vitasaidia mapato,” alisema.

Aidha, Jenerali Mabeyo alisema jeshi hilo linadaiwa na wazabuni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma hali ambayo inasababishwa na ufinyu wa bajeti.

Mkuu huyo wa majeshi alisema jeshi hilo lipo imara katika kulinda usalama wa nchi na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwao kwa maslahi ya nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo