Kwa haya ya Makonda, tuseme ‘hapana’


Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekuwa na `wakati mgumu’ akihusishwa na matukio yanayoibua mjadala kwenye jamii, kiasi cha kuwapo hisia za kutumia vibaya madaraka yake, hivyo anastahili ‘kupumzishwa’.

Yapo matukio mengi katika orodha yake yaliyofanywa ama kumhusisha Makonda. Si rahisi kuyataja yote kwa uhalisia wake yakatosha kwenye safu hii. Haiwezekani. Kwamba katika ujumla wake yanaibua hisia za watu ‘kumchoka’, wakitaka awajibike ama kuwajibishwa.

Rais John Magufuli akizungumza jana katika hafla kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Mandela na Morogoro, eneo la Ubungo, akagusia hisia za wananchi hususani wakazi wa jijini Dar es Salaam kumhusu Makonda.

Akasema yapo mambo mengi yanayozungumzwa na watu kumhusu Makonda, akiyaunganisha kuwa miongoni mwa hulka ya kujadili mambo binafsi badala ya masuala ya maendeleo, ambayo binafsi (Rais Magufuli) anaamini kuwa ndio msingi wa maendeleo.

Ni kweli, haiwezekani kupata maendeleo yaliyo endelevu kama wananchi ‘watakalia’ kuwajadili watu badala ya masuala. Pamoja na ukweli huo, lipo tukio moja ambalo hadi sasa linaweza kutajwa kuwa kilele cha yale yanayohusishwa na Makonda. Uvamizi wa studio za kituo cha redio na runinga cha Clouds cha jijini Dar es Salaam, akiwa na askari wenye silaha za moto.

Ni tukio linalodaiwa kutokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kuibua taharuki kwa viongozi na wafanyakazi wa kampuni hiyo ya habari, na baadaye umma mpana kufuatia kusambaa kwake kupitia mitandao ya kijamii.

Viongozi wa Clouds wameshalizungumzia na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, taarifa imeshawasilishwa polisi na viongozi kadhaa akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amelitembelea eneo la tukio na kuunda timu ya uchunguzi ya watu watano inayotarajia kutoa ripoti yake leo.

Wakati hali ikiwa hivyo, Rais Magufuli amemtaka Makonda kuendelea ‘kuchapa kazi’ na kwamba rai ya baadhi ya watu kumtaka amuwajibishe kwa kumuondoa kwenye nafasi hiyo, haiwezekani kwa vile hafanyi kazi kwa kuelekezwa na mtu, isipokuwa kufanya uamuzi pale inapofaa.

Hivyo inaweza kutafsiriwa kwamba Makonda amepata uhakika wa kuendelea kudumu katika utumishi wa umma akiwa Mkuu wa Mkoa, kwa maana ukweli unabaki kuwa hakuna shinikizo lolote linaloweza kumuondoa katika nafasi hiyo isipokuwa kupitia mamlaka za uteuzi ambazo zipo kwa Rais.

Pamoja na ukweli huo, ni wazi kwamba tukio la kuzivamia studio za Clouds unaomhusisha Makonda, mmoja wa viongozi vijana niliojuana nao kwa miaka kadhaa, akiwa na uwezo mzuri wa kujenga hoja, uamuzi na usimamizi, haukuwa sahihi. Unastahili kukemewa na kukaripiwa.

Uvamizi kama uliofanywa na Makonda utakuwa na madhara zaidi ikiwa utaachwa na kuenea kwa viongozi wengine wa Serikali hususani wakuu wa mikoa na wilaya, ama makamanda wa polisi na wengine wenye mamlaka za kuyaamuru majeshi ya ulinzi na usalama.

Clouds ni chombo huru cha habari, kilichoanzishwa kwa kufuata sheria za nchi, kikitimiza wajibu wake wa kuuhabarisha umma. Kinapotimiza wajibu wake kinyume cha sheria, zipo hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Lakini katika kutimiza wajibu huo, Clouds na vyombo vingine vya habari vinaongozwa na maadili na miiko inayotoa haki sawa ya kusikilizwa kwa pande zote zinazohusika kwenye habari yenye kulaumiwa kwa upande mmoja. 

Na inapotokea hali hiyo, mtoa taarifa hana mamlaka ya kulazimisha kwa namna yoyote, akiuelekeza utawala wa chumba cha habari kuitumia taarifa inayolenga ‘kumchafua’ mtu ama iliyo kinyume cha misingi, maadili na miiko ya uandishi ama utangazaji wa habari.

Inapodaiwa kwamba Makonda aliivamia Clouds ili kushinikiza, kisha kuchukua sehemu ya taarifa aliyotarajia kuiona ikirushwa katika mazingira yanayohusisha ushiriki wake katika kuiandaa, ili ‘imchafue’ kiongozi mmoja wa dini, haipendezi. Umma unapaswa kusema ‘hapana’.

Kwa maana kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa ikiongozwa kwa kuzingatia sheria, utawala bora na haki za binadamu. Moja ya misingi ya haki hizo ni uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza.

Makonda anapodaiwa kutaka kushinikiza kutangazwa kwa taarifa isiyokidhi mahitaji ya kimaadili katika tasnia ya habari, inaibua utamaduni wa mamlaka za utawala kutoheshimu asasi za kitaaluma zinazochangia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo na ustawi wa watu.

Mambo haya yanapojadiliwa haitoi maana ya kumchukia Makonda, la hasha. Bali kutoridhishwa na mwenendo wa vitendo vyake vinavyoibua uchungu na mkanganyiko kwa watu wakiwamo wanaomuamini kuwa ni mmoja wa viongozi vijana wenye uwezo wa kuongoza, lakini wakashindwa kuitumia vizuri fursa hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo