Waziri Mkuu Ethiopia kuwasili leo Dar


Celina Mathew

Haelemariam Dessalegn
WAZIRI Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Haelemariam Dessalegn, anatua nchini leo kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na kusaini mikataba mitatu atatembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Mikataba hiyo itahusu maeneo ya biashara na uwekezaji hususan kwenye utalii, viwanda na nishati ya mafuta huku mingine ikiwa ya kidiplomasia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Dk Suzan Kolimba alisema ujio huo ni mwaliko wa Rais John Magufuli.

Aliswema Rais alimwalika Dessalegn kwenye mkutano wa pembezoni mwa mkutano wa kawaida wa 28 wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia mwaka huu.

"Dessalegn anatarajiwa kuwasili asubuhi na atapokewa na Rais Magufuli na madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano mzuri kati ya nchi hizo pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ukiwamo uwekezaji na biashara," alisema.

Alisema wakati wa ziara hiyo, atafanya mazungumzo na Rais Magufuli na wajumbe wa pande mbili ambapo viongozi hao watashuhudia uwekaji saini mikataba ya ushirikiano kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Dk Kolimba alisema kesho ataendelea na ziara yake bandarini kujionea shughuli zinazofanyika na kisha wataondoka kurudi kwao.

Akizungumzia uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Dk Kolimba alisema ni mzuri na nchi hiyo imeonesha nia ya kufungua ubalozi   nchini hivi karibuni kwani sasa inawakilishwa na balozi wake aliye Kenya.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo