Polisi atakayetoa siri za wasiri kukiona



Salha Mohamed
Kamanda Lucas Mkondya
NAIBU Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya amesema Jeshi hilo litawafukuza kazi askari watakaotoa taarifa za raia wanaofichua wezi.

Mkondya alisema hayo hivi karibuni, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata malalamiko ya wananchi kwa baadhi ya askari kutoa taarifa za raia wema.

Mkondya alisema kama kuna askari anayepewa taarifa za uhalifu na kuzitoa atakamatwa, kufukuzwa kazi na kisha kupelekwa mahakamani.

"Tunampeleka mahakamani kwa sababu atakuwa amefanya kitendo cha uhaini cha kuhatarisha maisha ya raia mwema hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi," alisema.

Alisema endapo mwananchi ataona askari anayetaka kumpa taarifa hamfai basi aende kwa Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Siro.

"Kila raia aliye na taarifa za raia anayeona huyu matendo yake siyo, atoe taarifa mara moja ili Polisi ichukue hatua na kumkamata," alisema.

Aliwashukuru wenyeviti wa serikali za mitaa na viongozi na wananchi kutoa taarifa za wahalifu hadi mafanikio waliyopata katika kukamata wahalifu.

Mkondya alisema wananchi wanapaswa kutoa taarifa za watu wa mitaani kwao anayefanya vitendo vya kutilia shaka watoe taarifa.

Akizungumzia dawa za kulevya alisema ni lazima Jeshi hilo pamoja na wananchi kupambana kwa hali na mali kwani matumizi ya dawa hugharimu maisha ya vijana wa Taifa hili.

"Kila mwananchi kwenye mtaa wake atuletee taarifa na sisi tunamhakikishia tutazifanyia kazi kwa usiri mkubwa sana," alisema.

Alisema matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa yakirudisha nyuma uchumi wa nchi, hivyo ni muhimu kila mtu akapingana nayo.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi hilo kutaja wahusika huku akiwahakikishia kutotoa siri zao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo