Shikuba, wenzake wasubiri hatima rumande


Grace Gurisha

WAFANYABIASHARA watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, akiwamo Ali Hatibu Haji ‘Shikuba’, wanaendelea kusota rumande, wakisubiri rufaa waliyokata kupinga kuwekwa kizuizini ipangiwe Jaji atakayeisikiliza.

Rufaa hiyo iliwasilishwa juzi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na mawakili wa washitakiwa hao, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Ndusyepo alisema waliwasilisha rufaa yao, wanachokisubiri sasa ni namba ya rufaa hiyo na Jaji atakayeisikiliza, “hadi kesho tutajua nini kinaendelea”.

Watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel, ambao wote ni Watanzania.

Watuhumiwa hao wanapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kukubali maombi ya Waziri wa Sheria na Katiba ya kuwasafirisha Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa hizo.

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha alikubali washitakiwa hao wasafirishwe Marekani na pia aliamuru wakae rumande hadi Waziri wa Sheria na Katiba atakapopata kibali cha kuwasafirisha.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki kuwasilisha maombi hayo.

Wakati maombi hayo yanasikilizwa, Kakolaki alidai yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali Msaidizi wa Texas, Richard Magnes ambacho kilithibitishwa na kuapiwa kwa Jaji Nancy Johnson.

Kiapo hicho kinaeleza jinsi watuhumiwa hao walivyoshiriki kwenye mashitaka hayo, ambapo katika ushahidi ilidaiwa kuwa kuna mtu alipandikizwa kuchunguza wanavyoingiza dawa hizo Marekani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo