Shikuba, wenzake kukata rufaa leo


Grace Gurisha

Ali Hatibu Haji
WAFANYABIASHARA watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, akiwamo maarufu Ali Hatibu Haji ‘Shikuba’, wanatarajia kukata rufaa leo Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kupinga kuwekwa kizuizini kusubiri kupelekwa Marekani kushitakiwa.

Watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel, wote ni Watanzania. Rufaa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa mahakamani hapo kupitia mawakili wao, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu.

Mawakili hao walifikia hatua hiyo, baada ya kupata mwenendo wa maombi ya Marekani ya kuwahitaji kutokana na tuhuma za biashara za dawa za kulevya zinazowakabili nchini humo yaliyokuwa yakisikilizwa na kutolewa uamuzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

“Tutakata rufaa leo Mahakama Kuu, kwa sababu tayari tumepata mwenendo wa maombi ya wateja wetu, awali tulishindwa kufanya hivyo kwa kuwa yalikuwa bado hayajamalizwa kuchapwa,” alisema Ndusyepo.

Watuhumiwa hao wanapinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, kukubali maombi ya Waziri wa Sheria na Katiba ya kuwasafirisha Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa hizo.

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha alikubali washitakiwa hao wasafirishwe Marekani na pia aliamuru wakae rumande hadi Waziri wa Sheria na Katiba atakapopata kibali cha kuwasafirisha.

Uamuzi huo, ulitolewa baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki kuwasilisha maombi hayo. Wakati yanasikilizwa, Kakolaki alidai kuwa yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali Msaidizi wa Texas, Richard Magnes ambacho kilithibitishwa na kuapwa kwa Jaji Nancy Johnson.

Kiapo hicho kinaeleza watuhumiwa hao walivyoshiriki katika mashitaka hayo, ambapo katika ushahidi inadaiwa kuwa kuna mtu alipandikizwa kuchunguza jinsi walivyoingiza dawa za kulevya nchini humo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo