Papa Francis ataka viongozi wanyenyekee


VATICAN CITY, Italia

Papa Francis
KIONGOZI Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis. amewataka viongozi duniani kutenda mambo kwa unyenyekevu, huruma na upendo.

Kiongozi huyo wa kidini alizungumza kwa dakika 18 katika mkutano wa TED uliofanyika Jumanne Vancouver wenye kaulimbiu ya ‘Mustakabali Wako’– ikiwa ni mara ya kwanza mkutano huo kumshirikisha Papa.

Kwenye misa, alionya kuwa madaraka ni sawa na “kunywa pombe kali huku tumbo likiwa tupu”, na kusema kuwa viongozi na wanasiasa hawawezi kudhibiti mustakabali wa binadamu.

Akizungumza kwa Kiitaliano nyuma ya dawati, alianza: “Tafadhalini niruhusuni nizungumze kwa sauti na uwazi. Mnapokuwa na madaraka makubwa ndivyo pia vitendo vyenu vinapokuwa na athari kubwa kwa watu, lakini ndipo pia mnapotakiwa kuwa wanyenyekevu.

“Msipofanya hivyo, madaraka yenu yatakuharibuni, na ndivyo mtakavyoharibu wengine.” Aliongeza kuwa kuna usemi nchini Argentina usemao ‘madaraka ni sawa na kunywa pombe kali huku tumbo likiwa tupu.”

“Utajisikia kizunguzungu, unalewa, unapoteza mizania yako na utaishia kujiumiza pamoja na walio karibu yako, iwapo hutahusisha madaraka yako na unyenyekevu pamoja na upendo.

“Kupitia unyenyekevu na upendo wa kweli kwa wengine, madaraka – ya juu kabisa, yenye nguvu – yanakuwa huduma, nguvu milele. Mustakabali wa binadamu hauwezi kuwekwa mikononi mwa wanasiasa, viongozi wakubwa na kampuni kubwa.

“Ndiyo, wanabeba majukumu makubwa, lakini mustakabali kwa ujumla wake unakuwa mikononi mwa watu ambao wanatambua wengine kama ‘wewe’ na wao kama sehemu ‘yetu’.

“Sote tunahitajiana. Hivyo tafadhalini, fikirieni kwa upendo ili mkidhi jukumu mlilopewa kwa ajili ya kutenda mema kwa wengine – kwa kila mtu. Kwenu nyote na kwetu sote.”

Francis pia alitaka uwepo mshikamano mkubwa unaohusishwa na jitihada za kisiasa, kiuchumi na kisayansi.

Alisema ubunifu wa kiteknolojia ni mzuri, lakini si pale unapopofusha jamii za watu wanaoteseka.

“Itakuwaje faraja tutakapokuwa tunagundua sayari za mbali, na kuibua tena mahitaji ya ndugu zetu wanaotuzunguka,” alisema.

Papa alisema mara kwa mara hufikiria juu ya mababu na mabibi zake – wahamiaji kutoka Italia waliohamia Argentina.  Alisema anashangaa jinsi walivyoweza kuendana na ‘utamaduni wa upotevu’ katika dunia hii ya sasa isiyosamehe.

“Ningeweza kuishia kuwa mmoja wa watu wanaopuuzwa. Na ndiyo sababu siku zote najiuliza moyoni mwangu: ‘Kwa nini wao na si mimi?’”

Aliendelea: “Mtu mmoja anatosha kwa matumaini ya kuishi, na mtu huyo anaweza kuwa wewe. Kisha anaweza kuwapo ‘wewe’ mwingine, na ‘wewe’ mwingine, na kubadilika kuwa ‘sisi’.

“Hivyo, ina maana matumaini huanza pale tunapokuwa na ‘sisi’?” Hapana. Matumaini yalianza na ‘wewe’ moja. Kunapokuwa na ‘sisi’, hapo ndipo mabadiliko huanza.”

TED, kifupi cha Technology, Entertainment and Design (Teknolojia, Burudani na Usanifu), huandaa mikutano duniani kwa lengo la kubadilishana mawazo kupitia mazungumzo mafupi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo