LHRC: Bila Katiba Mpya nchi itakwama


Fidelis Butahe

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inapata suluhisho la kudumu la changamoto lukuki zinazolikabili Taifa, haziwezi kufanikiwa kama inavyotakiwa bila kuwa na Katiba Mpya.

Kufuatia umuhimu huo wa Katiba, kituo hicho kupitia Mkurugenzi wake mtendaji, Hellen Kijo Bisimba kimetoa mapendekezo manne ya kuendelea kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya uliositishwa mapema mwaka 2015 kupisha uchaguzi mkuu.

“…Masuala mengi ambayo yamelalamikiwa na wananchi na viongozi na hata juhudi za Rais Magufuli za kupambana na ufisadi, kuirudisha heshima ya watendaji serikalini yangeweza kupata suluhisho kwa kufufua mchakato wa Katiba Mpya ulioahirishwa bila tarehe maalum za kuurejesha,” alisema Bisimba.

Wakati LHRC ikieleza hayo Machi 31 mwaka huu Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi alisema Serikali imeanza kupitia sheria zinazohusika na Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kubaini utaratibu mzuri wa kuendelea na mchakato huo kwa hatua ya kupiga kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa.

Akieleza mapendekezo hayo, Bisimba alisema lazima Serikali iboreshe sheria zinazoongoza mchakato huo, yaani Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013 ili ziruhusu mwelekeo mpya wa mchakato huo.

“Maboresho haya ya sheria ni vema yakazingatia kuondoa vifungu vibovu vya sheria hizo ambavyo vimekua kivuli cha kuvurugika kwa muafaka katika hatua zilizopita za utungaji wa katiba mpya, ikiwemo kupunguza uwezekano wa wanasiasa na vyama vya siasa kuuteka mchakato wa Katiba,” alisema.

Alisema jambo la pili, wananchi wanapaswa kudai kurudishwa mjadala wa kitaifa juu ya haja ya kufufua mchakato huo kwa mrengo wa maoni ya wananchi na usitishwaji wa hatua inayofuata ya Kura ya Maoni kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni.

Alisema hali hiyo itatoa fursa kwa wadau kujenga muafaka mpya wa kitaifa na kuamua namna bora ya kuendelea hatua iliyobaki.

“Jambo la tatu ni Serikali kutenga bajeti kwa mwaka 2017/2018 kuwezesha mchakato huu kuendelea,” alisema.

“Nne, Serikali itekeleze maagizo ya hukumu inayohusiana na kura ya maoni iliyotolewa Februari 27 mwaka huu ili kuweza kuifanyia mabadiliko sheria ya Kura ya Maoni namba 11 ya mwaka 2013 itakayotoa muongozo wa kuendelea na mchakato wa katiba.”

Alisema tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba mwaka 2011, zaidi ya Sh bilioni 1 zimetumika na kubainisha kuwa ni aibu kutumia fedha nyingi kiasi hicho bila kupata Katiba.

“Kituo kinasikitishwa na ukimya wa Serikali juu ya kuuendeleza mchakato huu. Licha ya Serikali kusema mchakato utaendelea, lakini haikutengwa bajeti yoyote mwaka 2016/17,” alisema Bisimba.

“Kuwepo kwa kauli mbalimbali za viongozi ambazo zinakatisha tamaa, bado hakujarudisha nyuma jitihada za wananchi kudai mchakato huu kurejeshwa.”

Alisema pamoja na hatua iliyokwisha kufikiwa, LHRC kinaamini bado kuna fursa na wajibu wa kufanikisha kufufua mchakato huo ambao ulisusasua katika Bunge Maalum la Katiba baada ya baadhi ya wajumbe kugoma kushiriki.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo