Twaweza yabaini udhaifu kwa watoto


Suleiman Msuya

SHIRIKA la Utafiti la Uwezo la Twaweza, limebaini kuwa miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 13, wengi wao hawawezi kufanya majaribio ya kiwango cha darasa la pili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo kwa vyombo vya habari, takwimu hizo mpya zinaonesha mwenendo mzuri katika somo la Kiswahili katika shule za msingi, huku hali ya matabaka ikiendelea kujitokeza nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze katika taarifa hiyo alisema katika takwimu hizo wilaya ya Iringa Mjini, ilifanya vizuri kwa asilimia 74 ya watoto wenye miaka tisa hadi 13 kufaulu majaribio ya kusoma Kiswahili na Kiingereza na kufanya Hesabu.

Mkurugenzi huyo alisema wilaya ya Sikonge, asilimia 15 pekee walifaulu ambapo kimkoa, asilimia 64 ya watoto wa Dar es Salaam wenye umri huo walifaulu majaribio yote matatu, lakini mkoani Katavi asilimia 23 pekee ya watoto wenye umri huo ndio waliofaulu.

“Vilevile, asilimia 42 kutoka kaya masikini walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na asilimia 58 kutoka kaya tajiri. Tofauti hizi zinaonesha kuwa mahali anakoishi mwanafunzi panachangia kwa kiwango kikubwa matokeo ya kujifunza kuliko hali ya kiuchumi na vitu vingine ambavyo hudhaniwa,” alisema.

Kuhusu ufaulu, alisema utafiti ulibainisha kuwa hali hiyo inatia moyo kuona watoto wanapata matokeo mazuri zaidi kuliko miaka ya nyuma kwenye Kiswahili.

Alisema pamoja na ufaulu huo, safari bado ni ndefu kwa kile alichodai kuwa ni kukosekana kwa usawa kwenye matokeo ya kujifunza kuzingatia maeneo wanayoishi watoto.

“Takwimu zetu zinaonesha kuwa mahali anakoishi mtoto huchangia kwa kiwango kikubwa uwezo wa kujifunza, kuliko sababu zingine kama vile elimu ya mama, kupata ama kukosa elimu ya awali au kuwa na udumavu au la.”

Alisema matabaka yameendelea kujitokeza nchini ambapo alibainisha kuwa ipo tofauti ya asilimia 60 kati ya wilaya zinazofanya vizuri na zisizofanya vizuri

Alisema ripoti hiyo inatokana na takwimu zilizokusanywa na Uwezo Tanzania ambayo ni sehemu ya tathmini kubwa barani Afrika inayopima matokeo ya kujifunza ikiongozwa na wananchi.

Eyakuze alisema tathmini hiyo inatekelezwa pia Kenya na Uganda ambapo awamu ya sita ya ukusanyaji wa takwimu uliofanywa na Uwezo Tanzania mwaka juzi, jumla ya watoto 197,451 walifanyiwa tathmini kutoka kaya 68,588.

Alisema takwimu hizo zilikusanywa kutoka shule za msingi 4,750 na bado kiwango si kizuri kwa ujumla ikilinganishwa na matarajio ya mitaala katika masomo yote matatu.

Aidha, alibainisha kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa watoto wanaoweza kusoma hadithi ya Kiswahili katika darasa la tatu ni asilimia 56 na la saba ni asilimia 89.

Alisema wanaoweza kusoma hadithi ya Kiingereza, darasa la tatu ni asilimia 13 na la saba ni asilimia 48, wanaofanya Hesabu ni asilimia 35 kwa darasa la tatu na la saba ni asilimia 78.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo