Magufuli asamehe walioghushi vyeti


*Awapa mpaka Mei 15 kuondoka wenyewe serikalini
*Aagiza watakaobaki wakamatwe wafungwe miaka 7

Mwandishi Wetu

Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amesamehe kuwafikishwa mahakamani na kuwafunga miaka saba jela kwa watumishi 9,932, walioghushi vyeti, ikiwa wataacha kazi kabla ya Mei 15.

Alitoa kauli hiyo Dodoma jana wakati akipokea taarifa ya uhakiki wa vyeti bandia vya watumishi wa umma, akisema suala hilo kwa kiasi kikubwa limesababisha utendaji kazi mbovu, huku akionesha kushangazwa na viongozi waliopita kuacha suala hilo liendelee.

“Hatuwezi kuwa na Taifa la watu wasio na sifa, nafasi zitangazwe ili watu waombe … wanajijua, hivyo bora waondoke na watangazwe kwenye magazeti maana hao ni majambazi na mijizi kama mingine,” alisema.

Aliagiza pia kuwa watu hao 9,932 mishahara yao ikatwe na waondoke mara moja na watakaobaki baada ya Mei 15, vyombo vya ulinzi na usalama viwakamate na kuwafikisha mahakamani, ili wafungwe miaka saba kwa mujibu wa sheria.

Rais Magufuli alisema Tanzania haijasema inaajiri watu wenye Shahada, bali kuajiriwa kwake kunatokana na kiwango cha elimu alichonacho mwomba ajira, hivyo kuwataka waliofukuzwa kutafuta kazi zinazoendana na viwango vya elimu walivyosomea.

“Kila mtu aende panapomfaa, lakini kama mtu ameshindwa kufika sehemu anayotaka asiruke kwa kupita njia za mkato, bali ajiendeleze na si kudanganya, kwa kuwa ni kosa kubwa na adhabu ni kubwa,” alisema na kuongeza:

“Watakaojiondoa msiwapeleke mahakamani na hadi Mei 15 ambao watakuwa hawajaondoka wenyewe, polisi kamateni, wapelekeni wakajibu walipata wapi vyeti hivyo.”

Wanaoshirikiana vyeti

Kuhusu watumishi 1,538, ambao vyeti vyao vimekutwa vikitumiwa na watu zaidi ya mmoja, Rais Magufuli aliagiza wasilipwe mshahara wa mwezi huu, hadi wenye vyeti halali watakapojitokeza.

Alisema huenda idadi ya watumishi wasio na vyeti vinavyoendana na nafasi zao wakafikia 12,000 na kuagiza ajira zao zitangazwe na kupewa wanafunzi wanaomaliza vyuo na wanaohangaika kutafuta kazi, wakati wana sifa.

Ripoti

Awali wakati akisoma ripoti hiyo kabla ya kuikabidhi kwa Rais Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alifafanua kuwa kazi hiyo haikuwa rahisi, kwa kuwa walikuwa wanabezwa na watu kuwa kama sensa inaweza kuchukua hata siku mbili, kwa nini suala la vyeti limechukua muda.

Alisema taarifa hiyo iligawanywa kwenye makundi manne; la kwanza lilihusisha wenye vyeti halali 376,969 sawa na asilimia 94.2 ambavyo vilionesha magamba yao yalitolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) na taarifa zao zinafanana na zilizo kwenye kanzidata ya Baraza hilo.

Alisema kundi la pili lilihusisha watu walioghushi ambao ni 9,932 sawa na asilimia 2.4 ambapo vyeti vyao vilikuwa na magamba, alama za siri na  muundo ambao haufanani na vya Necta na baadhi taarifa zao zilifutwa na kuandikwa upya tofauti na zilizo kwenye kanzidata.

Kundi la tatu lilikuwa la vyeti vilivyotumiwa na mtu zaidi ya mmoja, ambao walikuwa 1,538 sawa na asilimia 0.3 huku watumishi wa umma 376 wakionekana kutumia cheti kimoja zaidi ya watu wawili hadi watatu.

“Kila jina la cheti linafanana na lililo kwenye kanzidata, wengine unakuta halijafanana kwa kuwa majina yanakuwa yameongezwa mwishoni, mwanzoni au limewekwa kifupi katikati na taarifa zao zinatofautiana na zilizo kwenye kanzidata,” alisema.

Kundi la nne ni vyeti vyenye upungufu, ambapo watumishi 11,596 walibainika kuwasilisha vyeti vya taaluma pekee na hawakuweka cha kidato cha nne wala sita.

Alisema hilo ndilo eneo pekee linalowapa shaka na wanajiuliza kama mtu huyo alipataje cheti cha taaluma na kuwataka waajiriwa hao kupeleka vyeti vya kidato cha nne au cha sita kwa waajiriwa wao.

Viongozi

Kabla ya taarifa hiyo na kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alitaka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kilichokuwa kikitimiza miaka 10 jana, kusoma kwa bidii kwa kuwa ndio wanaotazamiwa kuongoza nchi kwa miaka ijayo watakapoachiwa na viongozi wanaopita.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alimpongeza Rais kwa   kufanyia mkutano wake chuoni hapo ikiwa ni mara ya kwanza kwa kuwa waliitamani sana nafasi hiyo.

“Naomba nikiri kuwa tulikuwa tunapata wivu ulipokuwa unakwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tukawa tunajiuliza utakuja huku lini, hivyo mmekuja wote tumefurahi sana,” alisema na kuongeza.

Mimi ni msaidizi wako hapa Dodoma, nawafahamu wanafunzi wako vizuri anayesema wana matatizo ni majungu, wako ‘bomba’ wanatoa ushirikiano wameweka utaratibu mzuri, ndiyo maana hatujawahi kuzungumza chochote kuhusu hawa wananfunzi.

Aliongeza kuwa mkoa wake umeweka utaratibu wa kushirikiana na wanachuo, wanaohusika na afya, walimu barabara, hivyo wameweka  utaratibu kuhakikisha wanawasaidia ili wasisumbue kwenye ‘Boom (posho za mwezi)’.

Mkuu UDOM
Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Idris Kikula alisema hatua ya Rais kwenda chuoni hapo inaonesha namna anavyokijali licha ya kuwa na mambo mengi ya kufanya.

Alisema chuo hicho kinatimia miaka 10 tangu kilipoanzishwa kwa kudahili wanafunzi zaidi ya 40,000, hadi sasa kina vyuo saba na wanafunzi 23,163 ambapo wengine wanasomea shahada za awali wengine za juu.

“Kimesomesha wafanyakazi zaidi ya 400 kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani vya mapato na kupunguza idadi ya wanataaluma na gharaa kwa Serikali pamoja na kutoa ajira,” alisema.

Alisema mashine 10 zilipatikana kutoka kwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambazo zimeokoa wagonjwa wa figo zaidi ya 400 huku zaidi ya watu 500 wakipata huduma ya Ukimwi.

Aliongeza kuwa changamoto zilizokuwa zinasumbua ni uhaba wa walimu na maji, hali iliyosababisha wakapunguza kasi ya udahili ili kukabiliana nayo na kwa sasa mitambo imeshajengwa, hivyo udahili unaendelea kama kawaida.

Aidha, maandalizi ya kupandikiza figo kwenye hospitali ya Benjamin Mkapa yako tayari na wataalamu watakwenda Japan kujifunza wakirudi watafanya kazi hiyo.

Profesa Kikula alisema chuo pia kimeajiri na kusomesha wataalamu wa kuchunguza uhalifu unaotendeka kupitia mitandao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo