CUF ya Maalim yatangaza ‘kusafisha’ ofisi


Sharifa Marira, Dodoma

Maalim Seif Shariff Hamad
WANACHAMA wa CUF wasiomwunga mkono Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wametangaza kwenda kwa mbwembwe na kujidai katika ofisi za chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam Aprili 30 ‘kufanya usafi’. 

Usafi huo unahusu pia kusafisha watu wote ambao chama hakiwatambui akiwamo Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi yake, hivyo wanachama zaidi ya 7,000 wa nchi nzima watakuwa katika ofisi hiyo kufanya usafi na kuanza kazi rasmi. 

Hayo yalisemwa jana kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa na wabunge wa CUF wanamwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari.

Mbunge wa Temeke,Abdallah Mtolea alisema siku hiyo wanachama wa CUF walio wengi watafanya usafi kwani tangu Lipumba alipotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wasiomtambua hawajaenda ofisini hapo jambo linalosababisha ofisi hiyo kuvamiwa na genge la wahuni.

“Mnaona makundi yanakwenda kufanya fujo na kupiga watu na mle ndani kuna uchafu mwingi, hatutaki ofisi yetu iendelee kuharibiwa,’’ alisema Mtolea.

”Wazo hilo lilianzishwa na wanachama wa Temeke nikalikubali, lakini wanachama wa maeneo mengine baada ya kusikia wamelipokea na wanataka kushiriki, hivyo tutaondoa uchafu wote,’’ aliongeza.

Alisema wanachama hao watakwenda na mafagio, madekio na vifaa vingine vya usafi, hawapangi kufanya uovu siku hiyo na hakuna tukio la uvunjifu wa amani linalokwenda kufanyika.

Alisema kaulimbiu ya siku hiyo ni ‘Lipumba hakubaliki’ na wabunge wa CUF 40 ambao hawamwungi mkono kiongozi huyo, watahudhuria siku hiyo.

“Maana ya uchafu ni kitu chochote ambacho hakiko sehemu inayotakiwa, kwa hiyo kama kuna mtu hastahili naye yupo pale maana yake naye ni uchafu anatakiwa aondoke.

Alisema hakuna tamko lililotolewa na mtu yeyote kuwa wanachama ambao hawamkubali Lipumba wasifike ofisini nasi tunaokwenda ni wanachama halali, kama Lipumba anajitambua na anajiona ni Mwenyekiti, apokee wanachama na si kuwakimbia.

Akizungumzia kama tukio hilo halitaharibu kesi mahakamani ya kupinga uamuzi wa Jaji Mutungi wa kumrudisha Lipumba katika nafasi hiyo, alisema wana imani na Mahakama katika kutoa haki ya kesi hiyo na kwamba tukio hilo haliwezi kuharibu chochote kwani wanakwenda ofisini kwao. 

Mbunge wa Malindi, Ally Saleh alisema: “Ile ofisi ni yetu tunarudi kwenye ofisi yetu, si mahali pengine sasa wakati umefika kwenda ofisini na hivyo hatuwezi kuingia ikiwa chafu,tunasafisha ili tupate sehemu ya kufanyia siasa. 

“Uamuzi wetu CUF umefika wakati lazima twende katika ofisi yetu kuu ya Buguruni, tunataka kwenda mzofafa yaani kwenda kwa mbwembwe na kujidai,’’ aliongeza.

Akizungumzia tukio la kuvamiwa kwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa hivi karibuni, aliomba wote ambao hawakufurahishwa na tukio hilo, walaani na kwamba serikali haijaonesha kuchukizwa nalo.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo