Majaliwa aeleza siri ya Tz kufikia uchumi wa viwanda


Suleiman Msuya

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania itafikia uchumi wa viwanda iwapo nidhamu ya kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia vitapewa kipaumbele.

Aidha, alisema Serikali inahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii na kuondoa urasimu usio wa lazima.

Waziri Mkuu huyo aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya kuhusu mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za ofisi yake bungeni mjini Dodoma kwa mwaka 2017/2018 mwishoni mwa wiki.

Alisema mafanikio yoyote katika kujenga uchumi wa viwanda yataonekana kupitia misingi ya nidhamu kuanzia kwa wasimamizi.

Alisema anafarijika kwamba misingi wanayoendelea kujenga katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda.

Waziri Mkuu huyo alisema kuwa ustawi wa nchi na mafanikio ya mipango ya maendeleo vinategemea amani na utulivu hivyo, kila Mtanzania anapaswa kuweka nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya nchi ili mipango iweze kufanikiwa.

Alisema jukumu la kujenga uchumi wa nchi ni wajibu wa kila mwananchi, hivyo jamii inapaswa kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi kwa hiari na kufichua wakwepa kodi wote na wala rushwa.

“Ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya kazi na ubunifu.  Tujenge utamaduni wa kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa,” alisema.

Majaliwa alisema rasilimali zilizopo ipo siku zitaisha hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa uangalifu na kuepuke matumizi mabaya ya rasilimali kama vile maji, madini na misitu ili zinufaishe kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Aidha, aliomba jamii na watumishi kuongeze nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo linalolifanyika na kuzingatia matumizi ya muda na kuachana na tamaduni na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe.

Majaliwa alitoa rai kwa kila mwananchi kutoa ushirikiano katika vita ya dawa za kulevya kwa kufichua mtandao wa wahusika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo