JPM awapa ajira madaktari 258


Hussein Ndubikile na Joyce Kasiki

Rais John Magufuli
KUFA kufaana. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais John Magufuli kuamuru madaktari 258 kuajiriwa na Serikali baada ya uamuzi wake wa kutaka wakaajiriwe nchini Kenya kugonga ukuta.

Uamuzi huo umekuja siku 32 tangu ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dk. Cleopa Mailu kuliwasili nchini na kukutana na Rais Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa mkataba madaktari 500 wa Tanzania ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini, ombi ambalo lilikubaliwa.

Kitendo cha Rais Magufuli kuridhia madaktari hao kuomba ajira nchini Kenya kilizua taharuki nchini, huku wachambuzi wa masuala ya afya wakisema si jambo sahihi kwa kuwa nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari.

Lakini wakati taratibu hizo zikiandaliwa huku madaktari hao wakianza kufanya maombi, wananchi na madaktari nchini Kenya walifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa serikali yao.

Mahakama nchini Kenya ilishindwa kuondoa pingamizi ya kupinga Madakatri hao wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini jambo ambalo jana Serikali imesema Rais Magufuli ametaka madaktari hao waajiriwe nchini na kupangiwa vituo vya kazi haraka iwezekanavyo.

"Hatua hiyo imekuja baada ya pingamizi hilo kushindwa kuondolewa wakati tarehe ya utekelezaji wa makubaliano mikataba ya ajira ambayo ni Aprili 6 hadi 10 mwaka huu kupita hivyo kuilazimu Serikali kubadili uamuzi wake," alisema Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Alisema Machi 18, Wizara hiyo ilitangaza nafasi za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya na kwmaba mpaka kufikia Machi 27, jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa.

Waziri Ummy alisema baada ya kufanyika uchambuzi ilibainika kuwa madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi Kenya vikiwemo vya baadhi ya uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya Sekondari, vyuo walivyosoma na kuhitimu masomo, sehemu ambazo waombaji walifanya mafunzo ya vitendo, kutakiwa na umri usiozidi miaka 55.

Vingine ni usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika pamoja na kutokuwa mtumishi wa Umma, hospitali teule za Halmashauri na hospitali za mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali.

''Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa maombi ya kazi, kuandaa hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za madaktari na mkataba wa ajira kwa madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri madaktari kutoka Tanzania'' alisema Waziri Ummy.

Aidha, alisema Serikali itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kuwapeleka Madaktari hao Kenya.

Aliongeza kuwa kufuatia uamuzi huo majina ya madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika mtandao wa wizara hiyo pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo