Kituo chashitushwa wanahabari kupigwa


Celina Mathew

Dk Hellen Kijo-Bisimba
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeeleza kushitushwa na matukio yanayoendelea nchini, likiwamo la waandishi wa habari kupigwa kwenye mkutano wa CUF na kumpa mapendekezo matatu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini katika kuboresha demokrasia nchini.

LHRC imeeleza kwamba matukio hayo yanachochea uvurugaji amani na kumomonyoa misingi ya demokrasia iliyojikita nchini.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha ustawi mzuri wa vyama kwa kutatua migogoro ndani na baina ya vyama ili kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani na kudumisha ustawi wa demokrasia.

Mengine ni Serikali kuhakikisha usalama kwa raia wanapokuwa kwenye shughuli zao, ili kuepusha hofu kwa wananchi na vyama kutumia uhuru wao kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha uvunjifu wa amani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kwa kiasi kikubwa mlolongo huo wa matukio ukiendelea unaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Tukio la uvamizi kwenye mkutano wa ndani wa CUF uliosababisha kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi wa habari Mabibo, Kinondoni, limezidi kuzua mjadala katika jamii juu ya hatima ya hali ya usalama kwa Taifa. Tunatoa pole kwa waandishi wa habari, viongozi na wanachama wa CUF,” alisema.

Alisema wao LHRC wanaona ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya shughuli iliyokuwa ikiendelea na kwamba tukio hilo limezua hofu juu ya usalama wa wanahabari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo linazorotesha haki ya kupata taarifa.

“Tunaitaka Serikali kutofumbia macho matukio haya yanayoota mizizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha vitendo vya kihuni na kuruhusu uvunjwaji wa sheria kiholela na tunatamani jamii yenye kuheshimu na kulinda haki za binadamu,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo