Jamii itendee kazi wosia wa maaskofu

MAHUBIRI ya maaskofu katika ibada za Pasaka juzi yalikemea mambo kadhaa yanayoonekana kutaka kuota mizizi katika jamii nchini, ikiwamo matukio ya hivi karibuni ya utekaji raia na mauaji ya askari Polisi.

Pia walizungumzia harufu ya ufisadi unaotaka kulikumba Taifa katika taasisi mbalimbali, uliooneshwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na suala la mishahara hewa na vyeti bandia.

Katika mahubiri yao, maaskofu hao walieleza kuwa matendo hayo maovu hayafanywi na Wapagani pekee, bali hata wenye dini wakiwamo Wakristo, hivyo jamii inapaswa kuungana katika kuliombea Taifa wakati wa tafakuri hii ya kufufuka kwa Yesu Kristo.

Wakasema Pasaka inaadhimishwa kwa ufufuko, hivyo mwanadamu anapaswa kumkataa shetani na fahari zake zote, lakini wengi wamekuwa wakienda kinyume.

Maaskofu hao walifafanua kuwa endapo matendo ya mwanadamu yatakuwa ya giza, ina maana mtu huyo amekuwa mmisionari wa shetani na si Mungu, kwani Mungu anapendezwa na yaliyo mema.

Kauli za maaskofu hao zimekuja huku kukiwa na mjadala ulioibuka bungeni, kuhusu nani anahusika katika utekaji wa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Musa ‘Roma Mkatoliki’ na Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Sisi tunaamini kuwa kauli hii ya viongozi wa dini imekuja wakati mwafaka, kwani mambo hayo yote ya utekaji, mauaji ya polisi, vyeti bandia na mishahara hewa, hayajapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Hivyo tunatoa mwito kwa jamii kutendea kazi kauli hiyo ya maaskofu tukiamini kuwa kila mwanajamii ana nafasi sawa katika kuyatafutia ufumbuzi masuala haya.

Tunaamini kuwa wakati Serikali na vyombo vyake vya Dola vikiwa na jukumu la kuendelea kuwatafuta walioteka raia hao na kusaka walioua polisi mkoani Pwani, jamii ina wajibu wa kutambua wahalifu hao na kutoa ushirikiano wa ushahidi kama utahitajika.

Mchango wa jamii katika kusaka wahalifu upo katika ukweli wa hao wanaoitwa majambazi. Pia hao wanaoendelea kujineemesha kwa vyeti bandia wanafahamika kwa majina yao halisi mitaani.

Tunaamini kuwa kama jamii itaunganisha nguvu na ikafanya kazi kwa karibu na vyombo vya Dola katika kukabiliana na suala hilo, watu hao wasiolitakia mema Taifa letu watabainika na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Ifahamike, kwamba viongozi wa dini si watendaji, ila ni wawakilishi wa Mungu duniani, hivyo tuchukue mwito wao kama mwito kutoka kwa Mungu na tuufanyie kazi, linalowezekana leo lisingoje kesho. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo