Mimba tishio kwa wanafunzi Busega


Ahmed Makongo, Simiyu

TAKWIMU zinaonesha kuwa takribani wanafunzi 15 hadi 18 wa kike kati ya 40 wanaojiunga na kidato cha kwanza wilayani Busega mkoani Simiyu kila mwaka hukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito. 

Mbunge wa Busega Dk. Raphael Chegeni (CCM), alibainisha hayo katika mahojiano na  mwandishi wa habari hii yaliyohusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo jimboni humo, ikiwa ni pamoja na kutaka kujua hali ya elimu. 

Dk. Chegeni alisema kuwa kati ya wanafunzi wa kike 40 wanaoandikishwa kuanza kidato cha kwanza kila mwaka, takribani wanafunzi 15 hadi 18, wamekuwa wakikatisha masomo yao kwa sababu za ujauzito.

“Jambo hilo ndilo linalofanywa mtoto wa kike ashindwe kufikia malengo aliyojiwekea maishani mwake,” alisema

Katika kukabiliana na suala hilo, mbunge huyo alisema ameamua kuanzisha mkakati kabambe wa utekelezaji wa ujenzi wa hosteli za wasichana katika shule zilizoko pembezoni mwa jimbo hilo, ili kuwanusuru watoto hao wa kike.

“Ni hali ya kutisha sana maana kati ya watoto 40 wanaoandiskishwa kuanza kidato cha kwanza kati yao 15 hadi 18 ukatisha masomo yao. Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, nimeamua kuanzisha mkakati kabambe wa kujenga hosteli kwenye shule zilizoko pembezoni mwa jimbo letu hili  tuweze kuwanusuru hawa watoto wetu wa kike,” alisema. 

Alisema kuwa watoto wa kike wamekuwa wakienda ama kutoka shuleni kwa kutembea kwa miguu, umbali mrefu, ambapo wakiwa njiani wamekuwa wakikumbana na vishawishi vingi kutoka kwa wanaume.

Alisema kwa sababu hiyo, ameamua kusimamia ujenzi wa mabweni ya wasichana ili watoto hao walale shuleni badalaya kutembea umbali huo na kuendelea kupata vishawishi.

Dk. Chegeni alitaja shule ambazo tayari zimeshaanza utekelezaji wa mradi huo wa hosteli za wasichana kuwa ni Sekondari ya Ngasamo.

Alisema kuwa shule hiyo imekuwa ikipokea wanafunzi wa kata mbili za Imalamate na Ngasamo yenyewe. 

Alisema kuwa mradi huo wa hosteli pia utatekelezwa katika kata nyinginezo jimboni humo na kuongeza kuwa pia shule ya sekonmdari Mkula itakuwa imeingia katika mkakati huo hivi karibuni.

“Shule nyingine ambazo ziko kwenye mkakati huu wa kujengewa hosteli za wasichana ni Mkula, Malili, Kabita na Sogesca,” alisema.

 Alisema kuwa wapo wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamekuwa akiwatafuta kwa ajili ya kuchangia katika miradi ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa mabweni hayo.

Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Ubalozi wa Ireland, Canada na serikali kwa ujumla.

Dk. Chegeni pia alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wanaume wakiwemo walimu wanaowarubuni watoto wa kike na kufanya nao mapenzi, ambapo alisema kuwa katika jimbo hilo hawataki kuona mchezo huo unaendelea kuwepo.

Alisema kuwa wanaume wa aina hiyo wasithubutu kufanya mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kuwataka walimu kutekeleza wajibu wao wa kufundisha watoto na kufuata maadili ya kazi yao ipasavyo na siyo vinginevyo.

Aidha, aliwaomba wazazi na walezi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya dola kuhakiskisha wanaume wanaokatisha masomo ya watoto wao kwa kuwapatia ujauzito wanachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi mahakamani pindi wanapohitajika na chombo hicho cha kisheria.

Alisema kuwa wakati wote anakuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kuwekeza kwenye elimu, ambapo yeye binafsi amekuwa akitoa misaada mbalimbali kwenye sekta ya elimu,ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa vitabu kwenye shule ili kuhakikisha kila mwanafunzi anajitosheleza kwa kuwa na kitabu chake cha kujifunzia.

Kuhusu suala la madawati alisema kuwa wananchi walihamasika sana na kuhakikisha changamoto hiyo inamalizika na kila mwanafunzi anasoma akiwa amekaa kwenye dawati.

Alisema suala la maendeleo jimboni humo linagusa sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, maji, afya, miundombinu pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Dk Chegeni, miradi ya maji imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa jimboni humo, ikiwa ni pamoja mradi wa maji uliotekelezwa katika kijiji cha Lukungu na kwamba pia miradi mingine ya maji ikiwemo ya visima virefu nay a bomba kutoka katika ziwa Victoria inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali jimboni humo.  

Alisema kuwa mkakati wake mwingine ni kuhakikisha wananchi wote hususan akinamama wanajiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, ili waweze kujiinua kiuchumi, sanajali mkakati wa kuwepo na chuo cha ufundi jimboni humo, ili wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari na kushindwa kuendelea waweze kujiunga kwenye chuo hicho na kujipatia ujuzi wa fani mbalimbali na hatimaye kujiajiri wao wenyewe ama kuajiriwa.  

Mbunge huyo alisema kuwa katika suala la maendeleo ndani ya jimbo hilo hakuna cha itikadi za vyama vya siasa na aliwaomba wananchi wote jimboni humo, kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha wanajiletea maendeleo, kwa kushirikiana na serikali hii ya awamu ya tano chini ya rais wetu Dk. John Magufuli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo