Kigogo CUF atiwa mbaroni Dar


Leonce Zimbandu

Abdul Kambaya
WAKATI Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akilaani waandishi wa habari kuvamiwa na kushambuliwa, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imemkamata Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa Chama hicho, Abdul Kambaya.

Kambaya alikamatwa jana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo zilizotokea kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wilaya ya Kinondoni hivi karibuni.

Alikamatwa wakati pia Profesa Lipumba akiwasilisha barua yake kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, ikilaani kuvamiwa kwa waandishi wa habari katika tukio hilo.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema Kambaya ni miongoni mwa watu saba waliokamatwa kutokana na vurugu kwenye mkutano huo.

Wengine kwa mujibu wa Kamanda Sirro ni Hamisi Abdallah na Mtawa Rashidi, aliyetajwa kuwa mlinzi wa Profesa Lipumba na kwamba upelelezi umekamilika na jalada la uchunguzi limewasilishwa kwa Wakili wa Serikali tayari kufungua kesi mahakamani.

Kamanda Sirro alisema kesi zitakazofunguliwa dhidi yao ni mbili; ya kuvamia na ya kushambulia na kwamba majalada ya kesi zote yamewasilishwa kwa wakili huyo ili kufungua kesi baada ya kujiridhisha na upelelezi uliofanywa na Polisi.

“Tunaomba aliyemkata panga mwenzake aliyefahamika kwa jina   la Mohamed kujisalimisha Polisi, kwani hawezi kukimbia mkono wa Serikali, atapatikana tu,” alisema.

Aprili 22, watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo kwenye hoteli ya Vinna wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso na kofia, alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake na kusababisha wananchi wamzingire na kumshambulia.

Awali katika ufafanuzi wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, lakini vyombo vya Dola viko kimya.

“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti, wako kimya tu,” alidai.

Kuhusu barua ya Profesa Lipumba kwa uongozi wa TEF, Mwenyekiti huyo wa CUF alisema yeye binafsi na kwa nafasi yake katika chama hicho, analaani kitendo cha waandishi wa habari kupigwa wakiwa kazini.

Alisema yeye na viongozi wenzake, wanaamini katika siasa za demokrasia za ujenzi wa hoja na anatambua na kuthamini umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza demokrasia na uwajibikaji wa vyama vya siasa na vyombo vya Dola.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo