Mama Kikwete aanza na swali bungeni


Joyce Kasiki, Dodoma

Mama Salma Kikwete
MBUNGE wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM), ameuliza swali la nyongeza muda mfupi baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza na kuapishwa.

Katika swali hilo, Mama Salma ambaye ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alitaka kujua mpango mahususi wa Serikali kuongeza usambazaji huduma ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF), mkoani Lindi.

"Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaongeza wigo wa kutoa huduma kwa wananchi katika mpango wa Tasaf III wa kunusuru kaya masikini hususan kwa mkoa wa Lindi?” Alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Angelah Kairuki alisema tayari wamesambaza huduma hiyo kwa asilimia 70 mkoani Lindi.

"Hivi sasa imebaki asilimia 30 ambayo ni takribani wakazi 350,000 ambayo wanatarajia kuikamilisha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa (CUF), alitaka kujua kama Serikali haioni haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya masikini hasa ukizingatiwa upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yao.

Pia alitaka kujua ni vigezo gani vya uhakika vitatumika ili kupata kaya masikini ambapo katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alihoji kama Serikali haioni umuhimu wa kuwapa fedha TASAF kwa mkupuo hata wa miezi sita ili kuongeza tija.

Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Kairuki alisema mpango huo wenye madhumuni ya kuwezesha kaya masikini kuongeza kipato, fursa na kuinua kiwango cha matumizi yao, ni wa miaka 10 na unatekelezwa kwa vipindi vya miaka mitano kuanzia mwaka 2013-2023.

Waziri huyo, alibainisha kuwa vigezo vya kupata kaya masikini huainishwa na jamii katika mkutano wa hadhara unaoendeshwa na wawezeshaji kutoka halmashauri za wilaya na kusimamiwa  na viongozi wa vijiji, mtaa na shehia.

“Ruzuku inayotolewa kwa walengwa imeongezwa baada ya kufanyiwa mapitio kwa kuangalia hali halisi, hata hivyo, ieleweke kwamba viwango vinavyotolewa vilipangwa hivyo ili kata masikini iendelee kujishughulisha na kazi nyingine za kuongeza kipato na kutotegemea ruzuku pekee,” alisema Kairuki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo