Anayedaiwa kusafirisha wasichana aomba afutiwe kesi


Grace Gurisha

RAIA wa Kenya, Mary Amukowa, anayekabiliwa na kesi ya kusafirisha wasichana 10 kutoka Tanzania kwenda Kenya kuwafanyisha biashara ya ngono, ameiomba Mahakama imwache huru kwa madai kuwa kesi hiyo ni ya kutengenezwa.

Mary alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati akijitetea dhidi ya kesi inayomkabili yeye, rafiki yake Jackline Milinga na Simon Mgawe.

Mkenya huyo alidai kuwa yeye ni mfanyakazi wa kampuni ya simu ya Safaricom ya Nairobi, Kenya na aliajiriwa mwaka 2014 na alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Akiongozwa na Wakili Nehemia Nkoko, Mary alidai kuwa Septemba 4 mwaka juzi akiwa na Jackline walisafiri kwa basi la Modern Coast kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi, ambapo walikata tiketi wakakaguliwa mizigo na hati zao za kusafiria bila matatizo.

Aliendelea kujitetea kuwa alikuja Dar es Salaam kumtembelea Jackline na nchini hakuna mtu aliyekuwa anamfahamu zaidi ya huyo na walifahamiana mwaka 2001 wakiwa Bujumbura, Burundi.

Mary alidai walipofika Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania  akiwa ameshagongewa muhuri wa kutoka nchini akiwa kwenye foleni ya kusubiri kugongewa muhuri wa kuingia Kenya, maofisa Uhamiaji wawili wa Tanzania walimkamata Jackline wakisema wana shaka na hati yake ya kusafaria, kwa sababu ilikuwa ni ya kidiplomasia na baadaye wakabaini kuwa halali.

“Mimi niliomba tuachwe huru, walituchukua maelezo, wakatupa na hao wasichana 10, tulikaa siku nne Uhamiaji Makao Makuu lakini tulipohamishiwa Uhamiaji mkoa hawakuwa nao tena,” alidai Mary.

Pia alidai hajui wasichana anaotuhumiwa kuwasafirisha na wala hakuwahi kuwaona hadi siku Zulfa, Lea, Angelina na Amina walipopelekwa mahakamani kutoa ushahidi kwa upande wa mashitaka.

“Mashitaka haya ni ya uongo na kutengenezwa, sijawahi kusafirisha binadamu yeyote, mimi ni mfanyakazi wa Safaricom naomba Mahakama iniache kwa sababu tuhuma hizi ni za uongo,” alidai Mary.  

Mgawe alidai tuhuma hizo si za kweli kwani hajawahi kusafiri nje ya nchi wala kukusanya binadamu kwa lengo la kuwasafirisha, hivyo aliomba Mahakama naye imwache huru.

Baada ya washitakiwa hao kutoa utetezi wao, pande zote zilitakiwa kuwasilisha hoja za majumuisho za kuishawishi Mahakama iwaone wana hatia au la kabla ya Mei 11 ambapo kesi hiyo itatajwa.

Jackline, Mary na Simon wanadaiwa kuwa Septemba 4 mwaka juzi,   Magomeni na Makumbusho waliajiri wasichana 10 na kuwasafirisha.

Inadaiwa kuwa waliwaajiri Najma Suleiman, Leah Mussa, Zulfa Ally, Rahma Mohammed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi, Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Hussein na kuwasafirisha  kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa shughuli za ngono, huku wakijidai kuwa waliwapeleka kufanya kazi.

Inadaiwa wasichana hao wana umri wa kati ya miaka 18 na 22.




               

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo