Kinachotengenezwa leo, kitaiathiri nchi kesho



Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
WANAFALSAFA na wanataaluma wengine waliobobea katika masuala ya utawala, sayansi ya siasa na jamii wamewahi kutabiri, wakati mwingine kuelekeza namna bora inayofaa kulijenga Taifa lenye mwelekeo wa kuleta maisha bora na ustawi kwa watu wake.

Kwa mfano, mwandishi aliye raia wa Marekani, Toddy Stocker katika tungo za semi mbalimbali, amewahi kuandika katika tafsiri isiyo rasmi, uamuzi unaoufanya leo unaathiri matokeo ya kesho. Akimaanisha kila kinachofanyika kwa muda uliopo, kina madhara, yawe hasi ama chanya kwa matokeo yajayo.

Stocker aliandika semi nyingi zenye maana na maudhui tofauti. Semi zake hata sasa zinaendelea kuifundisha jamii pasipo kujali mipaka ya kijiografia, hali ya uchumi, ukubwa na uimara wa jeshi kwa nchi husika ama vinginevyo.

Inawezekana kukawapo tafsiri tofauti, lakini kwa mujibu wa usemi niliouwasilisha ukiwa miongoni mwa semi nyingi, Stocker anautahadharisha umma hasa watu wenye dhamana za uongozi, utawala, uwakilishi ama dhamana yoyote yenye maslahi kwa umma, kuwa makini katika kujadili na kufikia uamuzi.

Hoja ya Stocker inaweza kuwiana na falsafa ya Mgiriki wa kale, Plato alipozitaja sifa za kiongozi (akimaanisha mtu mwenye dhamana ya umma), kuwa ni pamoja na uwezo mkubwa wa kifikra katika kutafakari, kuchambua na kufanya uamuzi sahihi kuhusu jambo lolote linaloihusu jamii anayoingoza.

Kwa maana nyingine, uamuzi unaofanywa na watu waliokabidhiwa dhamana katika ngazi tofauti kwenye jamii, hata kuanzia familia hadi taifa, wanaguswa na nadharia hizo na nyingine zinazoweza kutajwa na zisitoshe kwenye ukurasa huu.

Kwamba kama Taifa, walio na dhamana kwa namna yoyote hapa nchini, wanapaswa kuheshimu umuhimu wa misingi ya siasa na fikra za watu, ili kuijenga jamii huru inayoshiriki katika kulijenga taifa.

Hivyo ‘leo’ ni wakati muhimu katika kuifanya ‘kesho’ ya Taifa iwe katika hali gani. Iwe katika hali ambayo Mwanafalsafa Mtakatifu Augustine wa Hippo katika karne ya tano, anaitaja kuwa ni ‘Jiji la Mungu’, lenye utii, upendo, umoja, mshikamano na mengine yanayofanana na hayo.

Ama ‘kesho’ ya Tanzania itakuwa ‘Jiji la Jehanamu’ kwamba inakuwa na watu wenye chuki, visa, uhasama, hujuma, ukosefu wa utii, vita na aina nyingine za mafarakano yanayoharibu maendeleo na ustawi wa watu.

Ili kuwa mfano wa ‘Jiji la Mungu’, wenye dhamana wanapaswa kuzitafakari na kuzifanyia kazi dhana za waandishi na wanafalsafa, japo niliowataja hapo juu, ambao pamoja na wengine wengi maono yao yanaendelea kuigusa hata jamii ya sasa.

Nimeyaandika kutokana na mfululizo wa matukio yanayoikabili nchi. Ni matukio yaliyoshamiri zaidi baada ya kuanza kwa mfumowa vyama vingi vya siasa, uliotanua wigo wa ufahamu wa watu kuhusu kushiriki katika uongozi, uwakilishi ama kunufaika kutokana na fursa mbalimbali za kidemokrasia na haki za binadamu.

Matukio ninayoyalenga hapa ni yenye kudhalilisha utu wa mwanadamu, kukiuka haki za raia na vitisho vinavyoweza kuibua hofu miongoni mwa watu, wakashindwa kutimiza wajibu wa kuijenga nchi inavyopaswa.

Matukio kama kushambulia, kujeruhi, kuua, kuteka na kutisha kwa namna tofauti, hayakuzoeleka kwa Watanzania wanaosifika katika kuendeleza misingi ya umoja, amani na utulivu vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Viongozi hao ambao wote wametangulia mbele za haki (Mwenyezi Mungu azidi kuwapumzisha katika usingizi wa amani-amina), waliiacha nchi ‘ikiwa moja’ licha ya kuwapo tofauti za mitazamo, itikadi na imani. Lakini hata kabla ya kifo chake, dalili za kuondoka kwa hali hiyo zilianza kuonekana zikiwamo ‘nyufa za Muungano’.

Miongoni mwa nyufa hizo ni ubaguzi ambao Mwalimu Nyerere alisema kama utaachwa uendelee, wabaguzi wakimaliza kuwabagua wenzao watarejea na kujibagua wenyewe. Madhara yake ni mafarakano.

Kwa muda mrefu sasa, mathalani wanasiasa hasa wa upinzani wamekuwa wakilalamika kutotendewa haki na watawala. Walilalamikia kunyanyaswa, kudhalilishwa, kubaguliwa, kuhujumiwa, kupata kejeli na kunyimwa haki za kidemokrasia.

Walilalamikia kunyanyaswa hasa waliposhiriki matukio kama mikutano ya hadhara, walidai kudhalilishwa ndani na Bunge na kupitia vyombo vya Dola kama ilivyokuwa kwa kadhia nyingine dhidi yao.

Miongoni mwao wakasema, malalamiko yao hayapaswi kupuuzwa kwa maana yanaweza kutoka kwao yakaelekezwa kwa kada nyingine, na baadaye kuingia katika mifumo wa nchi na hivyo kuifanya isiwe mahali rafiki kwa maisha ya watu.

Vilio vya wapinzani vilipozidi huku vikipingwa kwa hoja za watawala, vikazoeleka na kuonekana kuwa vya kawaida. Lakini hawakuchoka, waliendelea kulalamika.

Vitendo walivyofanyiwa wapinzani ama baadhi yake vikadaiwa kufanywa kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga, ingawa kwenye maeneo yao ya biashara. Vikaenea kwa waandishi wa habari na kada nyingine. Idadi ya wanaolalamika ikazidi kuongezeka.

Pamoja na matukio hayo, ndani ya vyama vya siasa kukaibuka vikundi vilivyopewa mafunzo yaliyobatizwa ‘ulinzi wa chama’. CCM wakawa na Green Guards, Chadema wakakijenga Blue Guards wakati CUF ikiwa na Red Brigade.

Vikundi hivi kwa namna tofauti vikatuhumiwa kushiriki mafunzo ya kujihami, kupiga na kujeruhi, lengo likiwa ni kutimiza malengo ya kisiasa yaliyo nje ya maslahi ya umma.

Wapo watu waliopigwa hasa nyakati za uchaguzi mdogo. Ilitokea Tarime, Igunga na Arumeru Mashariki. Wapo waliolalamika kwamba mwenendo wa vikundi hivyo haukuwa wenye kulielekeza Taifa katika misingi yake iliyojikita katika utu, umoja na mshikamano. Walioasisi walipuuza, wakanyamaza, wakaviendeleza ama kusaidia jitihada za kuviendeleza.

Ikaelezwa kwamba waliopewa mafunzo walipohitimu wakatimiza wajibu wao, japo kwa uchache wao kutokana na ufinyu wa kazi zilipojitokeza. Kuna taarifa kwamba kila kwa nafasi yake hakijui baadhi ya ‘walinzi’ waliopitia mafunzo kwenye vikundi hivyo hivi sasa wapo wapi.

Katikati ya hali hiyo, kunaibuka hulka ya kuteka watu, kuwatesa na kuwajeruhi. Yalishatokea kwa wanasiasa kama waliokuwa Mwakilishi wa Mkunazini, Salum Msabaha, kiongozi wa Chama cha Madaktari, Dk Steven Ulimboka, Mhariri wa gazeti la Mtanzania, Absalom Kibanda na hivi karibuni mwanamuzi wa kizazi kipya, Ibrahim Musa maarufu kama Roma Mkatoliki.

Wapo wengine waliowahi kukumbwa na kadhia kama zilizowakabili hao, hata kama taarifa zao hazikuandikwa, lakini ukweli unabaki kuwa ni matukio yasiyoistahili Tanzania na Watanzania.

Lakini kubwa zaidi ni kutishiwa kwa bastola kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kutangaza kumvua wadhifa huo.

Nape alikumbwa na kadhia hiyo aliposhuka kutoka kwenye gari lenye namba za Serikali, ikiashiria alikuwa bado hajakabidhi ofisi na mali za ofisi.

Yapo matukio mengi ambayo hayajaibuka ghafla. Yaliandaliwa, yakapikwa, yakatekelezwa katika vipindi tofauti na sasa yanaelekea kujikita kwenye mioyo na makusudi ya baadhi ya watu. Nchi inakwenda katika mwelekeo ambao haukuwapo awali.

Tunapolikumbuka onyo la Mwalimu Nyerere, kwamba ‘mkimaliza kuwabagua wale, mtajibagua ninyi wenyewe’ kadhalika vitendo vinavyotenegenzwa leo dhidi ya raia halali wa Taifa hili, vitaliathiri taifa katika siku ijayo ama zinazokuja.

Vitendo hivyo vinaweza kuwa vilivyohusishwa kwenye Makala haya, japo kwa mfano, ama vile vya hujuma za kisiasa.  

Ni lazima kila raia pasipo kujali nafasi yake kwenye jamii, atambua kwamba kila kinachotengenezwa leo kina athari kwa nchi. Ni vema zikawa athari chanya zinazotokana na matendo ya jana, nchi itasonga mbele.

+255754691540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo