JPM azindua ujenzi wa reli, atamba kutoyumbishwa


Celina Mathew

Rais Magufuli akizindua ujenzi wa reli
RAIS John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa kwenye kituo cha reli cha Pugu, akisema yeye ni dereva na hakuna wa kumyumbisha.

Magufuli jana alifanya uzinduzi huo utakaogharimu Sh trilioni 2.7 hadi kukamilika kwake.

Ujenzi wa reli hiyo mpya ya kisasa awamu ya kwanza ni wa kati ya Dar es Salaam na Morogoro  itakuwa ya pili Afrika kwa mwendo kasi wa kilometa 160 kwa saa, baada ya iliyoko Moroco.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli alijifananisha na dereva wa lori, akisema dereva mzuri siku zote hapaswi kusikiliza muziki unaopigwa ndani ya gari, bali huangalia gari linakoelekea.

“Mimi ni dereva mzuri, nimepakia waendaji wanaoimba, wanaotazama mbele, nyuma na ubavuni, kila mmoja anaimba wimbo wake, lakini kazi yangu si kusikiliza nyimbo zao, bali kuhakikisha gari linafika linakoenda. Nami nitaifikisha Tanzania inakostahili kufika kwa kuwa wanaopiga kelele ni wapiga dili,” alisema Magufuli.

Alifafanua, kuwa alipoomba kura kwa wananchi aliahidi kusaidia masikini kuondokana na hali hiyo na hakuna wa kubadili ajenda.

“Wabunge waliahidi majimboni, hivyo najua tunakokwenda, asitokee mtu akabadili ajenda tukaacha kujadili yaliyo kwenye Ilani ya Uchaguzi, tukajadili mambo yasiyo na maendeleo,” alisema na kuongeza:

“Mapambano ya kukuza uchumi na ufisadi ni magumu yana milolongo, hasa unapobadili watu wachache waliozoea maisha ya ufisadi kwa miaka 50 kwa kuwa Waswahili husema ‘samaki mkunje angali mbichi’, mimi namkunja sasa kabla hajakomaa, bora walalamike wachache wengi wafurahi.”

Kauli ya Rais Magufuli imekuja huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa watu wa kada mbalimbali kuhusu utendaji wa Serikali yake na hali ya maisha vikiwamo vitendo vya utekaji watu, vinavyoelezwa kukithiri nchini.

Akizungumzia ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli alisema umepangwa kukamilika ndani ya miezi 30 ukihusu ujenzi wa kilometa 300 ambazo kilometa 205 zitakuwa za njia kuu na 95 za reli ya michepuko ya treni kupishana na kupanga mabehewa.

Rais Magufuli alisema mradi huo utakuza biashara kati ya Tanzania na Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan, na utarahisisha kasi ya usafirishaji mizigo kutoka mikoa mbalimbali nchini, itakuza sekta ya  uchumi hususan za viwanda, mifugo, madini na uvuvi.

Pia alisema utasaidia malighafi kusafirishwa kutoka zinapozalishwa hadi viwandani, utakuza utalii kwa watu wanaotoka Afrika Kusini na nchi zingine kwa kutumia treni, kutunza barabara na kuongeza ajira.

Aidha, alisema walipotangaza zabuni, wakandarasi 40 walijitokeza, lakini kampuni ya Uturuki ilishinda hivyo mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 300 kwa ajili ya kuanza kazi.

Aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi haraka kwa kuwa fedha zipo na ikiwezekana ukamilike kabla ya miezi 30.

RAHCO

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Masanja Kadogosa alisema kutakuwa na vituo sita vya abiria na vidogo sita vya kupishana treni.

Alisema treni zitaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa saa mbili na baada ya kukamilika awamu zote tano za ujenzi, zitaweza kufika Mwanza chini ya saa 10.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kukamilika kwa mradi huo kutaboresha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanzania (TPA) kutoa mizigo kwa haraka na kufikia wateja, tofauti na ilivyokuwa awali, huku Watanzania 600,000 wakipata ajira za moja kwa moja.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo