Msomi ataka marekebisho ya sheria


Abraham Ntambara

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse, ameishauri Serikali kuwasilisha bungeni marekebisho ya Sheria ya Upigaji Kura ya Maoni ya Katiba Mpya ili kuendelea na mchakato wake kwani imepitwa na wakati.

Alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Baraza la Uongozi la Dini na Amani (IRCPT) akisema marekebisho hayo yatafanya mchakato huo uende vizuri.

“Vifungu namba nne na tano vya hiyo sheria vinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili mchakato uanze upya, vimepitwa na wakati,” alisema Dk Jesse.

Alisema maboresho hayo yanatakiwa kufanyika, kwani kwa sasa vifungu hivyo haviwezi kutumika kutokana na kwamba tarehe iliyopangwa kupiga kura ilishapita, kadhalika taratibu za kuendesha elimu ya mpiga kura haikufanyika.

Dk Jesse alieleza kuwa kutokana na hali hiyo inatakiwa kutangazwa upya tarehe ya kupiga kura ya maoni na kutoa muda kwa ajili ya elimu ya mpiga kura ili wanaounga mkono Katiba pendekezwa na wanaopinga waelimishwe juu ya wanachokiamini akisema baada ya hayo kufanyika ndipo kura ya maoni ifuate.

Alisema kutokana na kutoshiriki kikamilifu kwa wapinzani wakati wa kuijadili bungeni, Dk Jesse aliomba pia washirikishwe ili maoni yao mazuri yaongezwe kwa ajili ya kuiboresha Katiba hiyo.

Mkurugenzi, Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga alisema lengo la semina hiyo ni kuwafundisha viongozi wa dini, ili waweze kushiriki kikamilifu katika suala la kurudisha mchakato wa Katiba Mpya.

“LHRC ina makubaliano na IRCPT kurudisha mchakato wa Katiba Mpya, tuna makubaliano ya kufundisha viongozi wa dini ili wachukue nafasi yao kwa ajili ya mchakato wa Katiba, ulianza na kuishia katikati,” alisema Henga.

Alisema wanataka mchakato urudi ambapo inatakiwa makundi yaweze kuchukua nafasi katika kuishauri Serikali.

Mkurugenzi wa IRCPT, Thomas Godda alisema anatamani kile ambacho kilianza kifikie tamati, kwani mchakato wa Katiba uligharimu fedha nyingi ambapo alieleza kuwa angefurahi kama Katiba ingekamilika kabla ya 2020.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo