Wadau wataka Tume ichunguze


*Wasiwasi watanda nani leo nani kesho
*Wengi washangaa ukimya wa Serikali

Waandishi Wetu

KWA takribani miezi sita sasa, Taifa linatikisika kutokana na hofu iliyotanda miongoni mwa wananchi kwa matukio ya uvamizi na watu maarufu kutekwa kiasi cha kutojua nani aliye salama kila uchwao au nani atafuata uchao.

Hali hiyo imeibua wasomi ambao wameieleza JAMBO LEO kwamba Serikali inatakiwa kuunda tume ya uchunguzi kubaini ukweli wa matukio ya utekaji, wakieleza kuwa wajibu wake ni kulinda usalama wa raia na mali zao.

Tangu Agosti mwaka jana hadi jana zaidi ya matukio 10 ya utekaji na uvamizi yameripotiwa na vyombo vya habari yakihusisha watu mbalimbali, wakiwamo wanasiasa, wanahabari, daktari na wasanii.

Matukio hayo yameliteka pia Bunge linaloendelea Dodoma na mitandao ya kijamii ambako yanajadiliwa na wananchi huku baadhi ya wabunge wakiituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kuhusika.

“Hivi sasa kila mtu ana hofu mitaani. Wananchi hawajui nani atatekwa kesho. Serikali ijitathmini na kuchukua hatua, maana hali hii imezidi kwa kweli. Inanishangaza Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa kimya. Kwa nini hatoi kauli kuwatoa hofu wananchi?” Alihoji Richard Mbunda, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Hii maana yake Serikali imeshindwa kufuata mkataba namba moja kwa raia wake ambao unaitaka kuwalinda na mali zao. Mkataba huu huingiwa tu pale wananchi wanapochagua Serikali,” aliongeza.

Matukio

Kutoweka kwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben Saanane tangu Agosti 8 mwaka jana, kulianza kuibua maswali mengi, huku wanasiasa, hasa wa Upinzani wakivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia aliko msaidizi huyo  wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wakati sakata hilo likiwa halijapoa, Machi 23 aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitishiwa bastola, muda mfupi kabla ya kuzungumza na wanahabari kueleza hatua ya Rais John Magufuli kumwacha katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema aliyemtishia bastola Nape si polisi, lakini hakueleza ni nani.

Nape aliondolewa siku moja baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa tukio la kiongozi mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto na kulazimisha arushiwe mahojiano baina ya watangazaji wa kipindi cha Shirika la Umbea Duniani (Shilawadu) na mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye ameibuka kuwa mpinzani wa kiongozi huyo wa mkoa.

Machi 26, msanii Emmnuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’ alikamatwa na polisi akiwa Morogoro baada ya kutoa wimbo wa ‘Wapo’ ambao unaeleza uwepo wa watu wa aina tofauti katika jamii, wakiwamo viongozi wenye vyeti vya kughushi na kuuliza sababu za ‘jipu lililoiva kutotumbuliwa’.

Ney aliachwa na polisi baada ya Rais Magufuli kusema anaupenda wimbo huo.

Aprili 5, mwanamuziki ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu wakiwa katika studio za Tongwe, Dar es Salaam, walitekwa na watu wasiojulikana, tukio ambalo limezua maswali mengi kutokana na Waziri anayehusika na Sanaa, Dk Harrison Mwakyembe kuibuka kwenye mkutano wa mwanamuziki huyo na wanahabari.

Roma ambaye nyimbo zake nyingi zimekuwa na mashairi ya kuikosoa Serikali, alionekana siku tatu baadaye katika kituo cha Polisi Oysterbay, ambako alikwenda kuripoti tukio hilo.

Juzi, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary (CCM) alieleza bungeni kuwa ni muda mrefu hajaingia Dar es Salaam, kwa sababu alitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, akidai wabunge wamezidi unafiki, na kwamba katika kuwashughulikia ataanza naye.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alitoa ushuhuda kuwa ni mmoja wa waliotekwa na Usalama wa Taifa na kwamba yuko tayari kuvuliwa uanachama kwa kusema ukweli.

Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) akieleza mbele ya Bunge juzi kuhusu kutoweka kwa Saanane sambamba na ushahidi alionao kuwa Usalama wa Taifa unahusika, Tume ya Serikali ya Haki za Binadamu (THBUB) ilikemea matukio hayo ya utekaji.

Wachambuzi

“Kwa nini Tume isiundwe? Inaonekana watekaji hawa si watu wa kawaida. Si majambazi hawa kwamba wanateka watu ili wapate fedha. Inaonekana ni kikundi kinachofanya kazi maalumu.

“Tume itatueleza ni akina nani hawa watekaji. Kama ni vyombo vya ulinzi na usalama vinahusika basi tujue,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco).

Alisema Serikali inatakiwa kujitathmini kama inapaswa kuendelea kuwa madarakani kutokana na kushindwa kutoa tamko lolote juu ya matukio ya uvamizi na utekaji yanayoendelea nchini.

Katika ufafanuzi wake, Mpangala alisema Serikali ina njia nyingi za kupambana na watu wenye nia mbaya kutokana na kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama, huku akishangazwa na ukimya uliopo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu aliungana na Profesa Mpangala akitaka kuundwa tume ya uchunguzi.

“Wabunge pia wamependekeza jambo hili, nadhani ndicho kitu kinachopaswa kufanyika sasa. Tume hii ndiyo itatupa majibu sahihi,” alisema.

“Ni kama inavunja mkataba wake na wananchi wa kuwalinda kwa hali yoyote ile. Haiwezekani wasiwe na upande wa kusimamia. Haiwezekani Tanzania kuwa na matukio ya utekaji ambayo tumezoea kuyaona katika nchi za Mexico, Honduras na Colombia,” aliongeza.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo