Mwigulu: Dini zisitumike kufanya uhalifu


Suleiman Msuya

Mwigulu Nchemba
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameonya waumini wa dini nchini kuacha kutumia mwavuli wa dini kufanya vitendo vya uhalifu ikiwamo kudhuru maisha ya wengine, huku akitangaza kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada.

Mwigulu alitoa onyo hilo juzi kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, akisema Serikali haitavumilia watu wa aina hiyo.

Alisema Serikali inatambua uhuru wa kuabudu iliyoutoa kwa wananchi wake na inaunga mkono kazi nzuri inayofanyika kupitia ibada, lakini uhuru huo usikwaze wengine wala usivunje sheria.

"Ucha Mungu si udini", hivyo ni sahihi kwa waumini kumcha Mungu kwa kiwango wanachopenda, lakini si kuwashikia silaha watu wengine ili wajiunge na dini zao.

“Wale ambao watatumia misimamo iliyopitiliza kudhuru maisha ya watu wengine, Serikali itasimama na kuwahesabia kuwa ni waovu na tutashughulika nao kama wahalifu wengine,” alionya.

Nchemba aliagiza taasisi zilizo chini ya wizara yake, kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada, badala ya kuwapa njia ngumu kwani nyumba hizo ni muhimu kwa ajili ya kuombea viongozi na Taifa.

"Elekezeni watu wanaotaka kusajili nyumba za ibada watimize masharti na muwasajili, hatuwezi kuweka masharti magumu ya kusajili nyumba za ibada halafu tukaweka masharti rahisi ya kusajili baa na kumbi za disko," alisisitiza.

Pia alitumia nafasi hiyo kuhakikishia wasanii wa nyimbo za Injili kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kulinda maslahi ya kazi zao, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo