Sumaye achambua awamu ya 3 na JPM


*Aeleza tofauti ya Ukapa na kusoma namba
*Asema haukudumu muda mrefu kama sasa

Celina Mathew

Frederick Sumaye
WAZIRI Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amechambua tofauti ya mazingira ya utawala wa awamu ya tatu, ambao ulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa fedha na kinachotokea sasa maarufu kusoma namba.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Sumaye alisema kuna tofauti nyingi lakini akaamua kuzungumzia kubwa zaidi kwa kujikita katika mambo mawili; moja ni uchumi na lingine demokrasia na utawala bora.

Sumaye ambaye ndiye Waziri Mkuu mwenye historia ya kukaa miaka kumi mfululizo katika nafasi hiyo, alisema katika Awamu ya Tatu Serikali iliimarishwa uchumi na kukuza na kuboresha nguzo kuu za uchumi, kwa kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuingiza ushindani wa kweli katika biashara.

Kwa mujibu wa Sumaye ambaye sasa ni kada wa Chadema, Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa,  ndiyo iliyojenga na kubuni vivutio kwa wawekezaji wa ndani na wa nje na kuanzisha ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP) katika uwekezaji.

Sumaye aliendelea kueleza kuwa Awamu ya Tatu, ambayo hali yake ya kukosena kwa fedha ilipewa jina la ‘Ukapa’ ndiyo iliyobuni na kuboresha miundombinu ya uchumi kwa kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji (TIC) pamoja na kuboresha sheria zilizoendana na uchumi huria na wa kisasa.

Alisema hata maboresho ya miundombinu ya barabara, bandari na maji yalianzia Awamu ya Tatu na katika huduma za jamii hasa elimu, awamu hiyo ndiyo iliyobuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), uliopeleka watoto wote wenye umri wa kuanza shule darasani na Mpango wa Maendeleo ya Elimu Sekondari (MMES).

“Awamu hii mengi ya mambo haya ni kinyume kabisa au hayatiliwi mkazo. Kwa mfano Serikali imekwishatamka kuwa kuanzia mwaka huu wa fedha idara za Serikali hazitapewa huduma na sekta binafsi. Hii ni kinyume kabisa na sera ya PPP,” alisema.

Alisema hata sera ya utozaji kodi, inapaswa kujenga uhusiano mwema baina ya mlipakodi na mtozakodi, lakini cha kushangaza hazishabihiani na badala yake wafanyabiashara wengi wamefunga biashara zao. 

Upatikanaji wa fedha

Akizungumzia hali ya upatikanaji fedha iliyopewa jina la ‘Ukapa’, Sumaye alisema Awamu ya Tatu ilipoanza, hali ya uchumi ilikuwa duni na fedha zilikuwa mikononi mwa wenye uchumi usio rasmi au uchumi wa magendo.

Alisema kazi ya kwanza ya Awamu Tatu, ilikuwa kurudisha uchumi katika misingi sahihi na katika kufanya hivyo walikubaliana kuua biashara ya magendo.

Alieleza kuwa kipindi hicho ndiyo watu wengi walipoona ugumu wa fedha kupatikana wakauita 'Ukapa', lakini kipindi hicho hakikudumu muda mrefu, kwani uchumi ulirudi katika misingi bora na kuimarika na watu wakaanza kupata fedha kulingana na jasho lao halali.

Demokrasia

Sumaye alisema Awamu ya Tatu pia ilikuza demokrasia na utawala bora na idadi ya vyama iliendelea kukua na vyama vya siasa vilifanya kazi za kisiasa kwa uhuru bila kuzuiwa au kungiliwa.

Alifafanua kuwa utawala bora wakati wa Awamu ya Tatu, ulikuwa wa 'ukweli na uwazi na uliofuata sheria’ na kutolea mfano wa nguzo tatu za dola ambazo ni Utawala, Bunge na Mahakama kwamba zilifanya kazi kwa uhuru bila nguzo moja kuingilia nyingine.

Waziri Mkuu huyo alisema watu walikuwa huru kutoa maoni yao bila wasiwasi wala kamata kamata au watu kupotea bila maelezo yoyote kutoka vyombo vya dola. 

“Awamu hii ni kinyume kabisa na hivyo. Demokrasia imekandamizwa kiasi kwamba vyama siasa havina uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara kama sheria inavyotaka na uhuru wa vyombo vya habari umeminywa kabisa. Mikutano ya Bunge haioneshwi tena mbashara katika luninga kama zamani,” alisema.

Aliongeza kuwa hayo yote yanavunja Katiba ya nchi ibara ya 18 kwa sababu ni haki ya kikatiba wananchi kuwa na uhuru wa kutoa, kupata au kusambaza habari.

Alisema kwa sasa ni jambo la kawaida wapinzani kukumatwa bila sababu za msingi na kukaa rumande muda mrefu kuliko saa 48 zinazoruhusiwa kisheria na hata wengine kufungwa jela.

Kwa mujibu wa Sumaye, hata kupotea kwa watu wenye mawazo tofauti na Serikali au 'kuvamiwa na watu wasiojulikana' kumeanza kuwa jambo la kawaida.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo