Wanahabari watakiwa kuibua mijadala


Hussein Ndubikile

VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kujenga utamaduni wa kuibua mijadala itakayosaidia kuiletea nchi maendeleo huku vikisisitizwa kuacha kusubiri ajenda za mipango ya maendeleo kutoka kwa wanasiasa.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Theophil Makunga wakati wa utoaji taarifa ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani itakayofanyika Mei 2 na 3 Mwanza.

Alisema katika jamii kuna mambo mengi yanayotakiwa kuibuliwa kwa kuyasemea ili kufanyiwa kazi na mamlaka husika, hivyo ni vema vyombo hivyo vikajikita kutatua matatizo yanayokabili wananchi.

"Duniani kote, tabia za vyombo vya habari hubadilika hivyo lazima vyombo vyetu vibadilike, tusigonje ajenda za wanasiasa zije kwetu, tunatakiwa kugusa matatizo yanayoigusa jamii," alisema Makunga.

Alisisitiza kuwa vyombo vya habari vinatakiwa kuyapa umuhimu matatizo ya kijamii huku akitaka kuitumia siku hiyo kupiga kelele ya kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unapatikana.

Aliongeza kuwa nchi zingine suala la uhuru wa vyombo liko katika hali mbaya na kwamba hali hiyo haitakiwi kuvirudisha nyuma kuendelea kudai haki hiyo.

Makunga alisema suala la vyombo vya habari kusubiri ajenda za Serikali lilikuwapo lilipotangzwa Azimio la Arusha na Azimio la Iringa na kwamba wakati huu waandishi wa habari wanatakiwa kubadilika kuendana na hali iliyopo.

Awali akizungumzia kuelekea Siku hiyo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika (MISA), Salome Kitomari alisema zaidi ya washiriki 250 wa ndani na nje ya nchi wamealikwa.

Alisema atakuwapo pia Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni,   Dk Harrison Mwakyembe, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya nchini, mabalozi, wabunge,  wakuu wa asasi zisizo za serikali za kitaifa, vyuo vya uandishi wa habari, wanachama wa vyama vya kijamii na waandishi wa habari wakongwe.

Alifafanua kuwa masuala mbalimbali yatajadiliwa yakiwamo ya lengo la kufikia makubaliano ya kitaifa kuhusu utaratibu wa usalama na ulinzi wa wanahabari na wafanyakazi wa vyombo hivyo kwenye mitandao na nje ya mitandao na kuweka msukumo kwa mataifa kutunga sheria rafiki za vyombo hivyo zitakazohakikisha uhuru katika nchi husika.

Aidha, alisema wakati wa maadhimisho hayo, wahanga wa ukiukwaji wa uhuru wa habari watatoa ushuhuda kuhusu changamoto walizokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao.

Salome alisema siku hiyo Ripoti ya vyombo vya habari vya Kusini mwa Afrika iliyoandaliwa na MISA inayojulikana kwa jina la ‘Kwa hiyo hii ni Demokrasia’ itazinduliwa pamoja na mfululizo wa taarifa ya UNESCO ya sera za vyombo vya habari vya kijamii.

Mwakilishi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Razia Mwawanga alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni fikra yakinifu kwa wakati mwafaka, huku akibainisha kuwa waandishi wanahitaji kufanya kazi zao bila kuingiliwa.

Alisema Mfuko huo umefanya kazi kubwa ya kuwezesha waandishi wa habari 40 wa vyombo 13 kuandika habari zilizochangia uwajibikaji.

Mwakilishi wa Klabu za Umoja wa Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Jane Mihanji alitaka waandishi kuchukua hadhari wanapokuwa kwenye kazi zenye mazingira hatarishi na kuwasisitiza kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa.

Mwakilishi wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNDP), Stella Vuzzo alisema siku hiyo ina umuhimu kwa kuwa inatambuliwa na Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wanahamasishwa kuiadhimisha.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo