Mashamba, skimu zapigwa faini ya mamilioni


Mwandishi Wetu

Shamba la mpunga
MASHAMBA ya mpunga matatu na skimu tatu za umwagiliaji zimetozwa faini ya jumla ya Sh milioni 120.3 kwa ukiukaji wa sheria za mazingira chini ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC).

Mashamba hayo ni ya Mbarali Highland Estates, Kapunga Rice Project na Kapunga Small Holders huku skimu za umwagiliaji zikitajwa kuwa ni za Mwanavala (Nguvukazi), Mwashikamile na Mwendamtitu zilizoko Mbarali, Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa Kikosikazi cha Kitaifa cha Kuokoa Ikolojia ya Mto Ruaha, Richard Muyungi, alisema makosa yaliyokutwa katika mashamba hayo ni pamoja na kukosa vyeti vya ukaguzi wa mazingira.

Lakini pia kukiuka taratibu za umwagiliaji kwa kutoa na kutumia maji bila ruhusa, kuweka mifereji mikubwa ya kumwagilia mashambani bila kufuata sheria na kanuni zinazotakiwa na kutorekebisha miundombinu ya umwagiliaji kwa mifereji ya kutolea maji.

Faini hiyo inayotakiwa kulipwa ndani ya siku 14 kuanzia juzi, ilitozwa na Kikosikazi hicho kupitia Mwananasheria wa NEMC, Vicent Haule, baada ya kugundua makosa hayo ya uvunjifu wa sheria za mazingira.

Kwa mujibu wa Muyungi Mbarali Estates inatozwa Sh milioni 33, Kapunga Rice Project Sh milioni 33.1, Kapunga Small Holders Sh milioni 3 huku Madibila ikitozwa Sh milioni 33.

Skimu za umwagiliaji za Mwendamtitu Sh 7,995,000, Mwanavala (Nguvukazi) Sh 7,995,000 na Mwashikamile Sh milioni 2.2.

Aidha aliongeza kuwa mashamba ya Mwashikamile, Mwanavala na Kapunga Small Holders, wanatakiwa kulipa faini lakini pia baada ya kuvuna watatakiwa kuacha kulima katika mashamba hayo mpaka watapofuata taratibu za vibali vya maji na cheti cha ukaguzi wa mazingira kutoka NEMC na Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji.

"Kutoza faini hizi si kukomoa mashamba ila ni kuhakikisha kuwa wamiliki wa mashamba makubwa ya umawagiliaji nchini wanafuata taratibu na sheria za mazingira katika kuendesha mashamba hayo," alisema Muyungi.

Kikosikazi hicho kiko Mbeya kukagua na kutembelea sehemu za mashamba, skimu za umwagiliaji na kusikiliza maoni ya wananchi ikiwa ni harakati za kurudisha ikolojia ya Mto Ruaha.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo