Utafiti wa awali mafuta Z’bar wakamilika


Juma Mohammed, MAELEZO Zanzibar

Ali Khalil Mirza
KAZI ya awali ya utafiti wa utafutaji na uchimbaji wa  mafuta na gesi asilia kwa kutumia ndege maalum imekamilika visiwani Zanzibar, na sasa taarifa za utafiti huo zimepelekwa  Edinburgh Uingereza kwa ajili ya utambuzi wa kitaalam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Ali Khalil Mirza, alisema   kazi hiyo imekwenda vizuri na watafiti hao walijiegemeza zaidi katika kitalu cha Pemba- Unguja ambako waliruka kila siku kwa muda wa saa sita.

“Huu ni utafiti wa awali, nachukua fursa hii kuwajulisha kwamba wataalam wetu wamekamilisha kazi na wamefanikiwa kukusanya taarifa za kutosha kuhusu rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar,” alisema Mirza.

Katibu Mkuu huyo alisema awali kazi hiyo ilipangwa kufanyika kwa   miezi miwili, mwezi mmoja ndio utafiti wenyewe, lakini wakaweka na mwezi mwengine ikiwa kutatokea dharura yoyote ambapo haikutokea na hivyo kukamilisha ndani ya wiki tatu.

Kiongozi wa timu ya watafiti kutoka kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna alisema wamekamilisha kazi yao na kilichobakia ni taarifa zilizokusanywa kuwasilisha Uingereza kwa ajili ya uchambuzi wa kitaalamu.

Stefan alisema kuwa wametumia wiki tatu kufanya kazi hiyo tofauti na makisio ya awali ya miezi miwili, kutokana na kuanza kwa kipindi cha mvua za masika.

“Ndege yetu ina vifaa ambavyo havihitaji vishindo, kama tutaruka wakati wa mvua na ngurumo za radi, inaweza kurekodi kitu ambacho sisi hatukihitaji katika utafiti wetu ndio sababu ilitulazimu kufanyakazi muda mrefu Zaidi,” alisema mtaalamu huyo.

Kiongozi huyo wa timu ya wataalamu, alisema kazi yao ilikuwa kukagua miamba iliyoko chini ya ardhi ambapo kwa kitaalamu inajulikana “Airborne Full Tensor Gravity Gradiometry Survey” (FTG).

Stefan alisema katika kitalu cha Pemba -Zanzibar wameona chembechembe ya mafuta, lakini taarifa zaidi ya kuwepo kwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia itapatikana baada ya kukamilika kwa   uchambuzi wa taarifa yao watakayoiwasilisha Makao Makuu ya Kampuni ya Bell Geospace ya Uingereza.

Alisema kazi ya uchambuzi wa taarifa za kitafiti walizokusanya itakamilika ndani ya mwezi mmoja na wataikabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Falme za Kiarabu.

Mtaalamu wa masuala ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta kutoka Kampuni ya ya RAKGAS ya Ras Khaimah, Graham Cunningham ambaye pia ni Meneja wa Mkaazi wa RAKGAS Zanzibar, alisema kimsingi kazi iliyoko mbele ni kubwa zaidi kwani huo ni utafiti wa awali tu.

“Kuna kazi kubwa mbele yetu, utafiti huu uliofanywa, utatusaidia kujua object iliyopo, lakini kazi bado inaendelea,” alisema mtaalam huyo.

Alisema katika miezi mitatu au mine, wanatarajia kuanza awamu ya pili ya utafiti kwa kutumia meli maalum itakayofanya utafiti katika mwambao wa pwani ya Zanzibar katika kitalu cha Pemba-Zanzibar.

Mtaalamu huyo alisema pia utafiti huo utahusisha gari maalum litakalotafiti maeneo ya ardhini katika sehemu ambazo taarifa zake zimetolewa katika utafiti wa awali uliofanywa na ndege ya Kampuni ya Bell Geospace.

Kamapuni hiyo ya kigeni inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya  Brunswick Zanzibar Limited inayohusika na shughuli za uombaji wa vibali kutoka serikalini kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo