Uyoga wenye sumu waua 3 Tanga


Mwandishi Wetu, Tanga

WATU watatu wamefariki dunia na wengine watatu kulazwa kwenye hospitali ya Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Songe wilayani Kilindi mkoani hapa.

Kadhia hiyo imetokana na kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu nyumbani kwao kijijini Mabalanga wilayani hapa, Aprili 22.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba jana aliwataja marehemu kuwa ni Rahma Athumani (5) ambaye alifariki dunia usiku wa Aprili 22 baada ya kufikishwa katika zahanati ya Mkuyu na kaka yake, Ramadhani Athumani (6) aliyefariki dunia siku iliyofuata.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mabalanga, Ramadhani Maudo alisema jana kwa njia ya simu kwamba mtu mwingine, Zaina Mbwana (36) alifariki dunia juzi mchana na kuzikwa jana kijijini hapo kutokana na tatizo hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Wakulyamba alisema tukio hilo lililohusisha watu wa familia moja lilitokea siku hiyo, baada ya watoto hao kwenda porini kutafuta mboga na kuchuma uyoga huo na walipofika nyumbani usiku, wazazi waliupika na kula.

"Inavyoonekana, wazazi hawakutazama vizuri uyoga huo, walipoletewa na watoto wale, waliuandaa na kuula ndipo walipojisikia vibaya na kukimbizwa kwenye zahanati ya kijiji cha Mafleta kata ya Jaila, kwa matibabu na kuhamishiwa katika hospitali ya KKKT," alisema.

Kamanda aliwataja waliolazwa kuwa ni Mahija Athumani (9) ambaye anasoma darasa la pili katika shule ya msingi Mabalanga, Mariamu Athumani (33) na Aziza Toba (13) ambao wanaendelea na matibabu.

Alisema wataalamu wa afya wanaendelea kuchunguza kujua aina ya sumu iliyokuwa kwenye uyoga huo ambao watoto hao waliuchuma porini kama ilivyo desturi ya watu kula uyoga unaojiotea porini.

Katika tukio lingine, polisi mkoani hapa wanachunguza kifo cha Mariam Bernado (43) ambaye Aprili 21 alikutwa amekufa maji kwenye bwawa   lililopo Handeni baada ya kutoweka nyumbani kwao usiku.

Alisema mwanamke huyo anayeishi nyumbani kwa mwalimu Gerard Moroma wa shule ya msingi Msasa, alitoweka nyumbani usiku kabla ya kukutwa asubuhi akiwa amekufa bwawani humo ambalo linatumiwa na wananchi wa Chanika.

Kamanda Wakulyamba, alisema taarifa za awali za mama huyo zilisema alikuwa na matatizo ya akili ambayo yanadaiwa kutokea baada ya kifo cha mumewe aliyemwachia watoto watatu anaoishi nao kwa mwalimu huyo.

Katika tukio lingine, mfanyabiashara Mohamed Ally (35) wa kijiji cha Mapanga tarafa ya Kwekivu wilayani Kilindi amevamiwa na majambazi wenye bunduki aina ya magobori wakimtaka awape fedha, lakini alipowaeleza hana, walimfyatulia risasi mbavuni na kumuua.

Kamanda wa Polisi alisema polisi inashikilia watu wanne kuhusu tukio hilo na pia wanaendelea kusaka watu wengine waliohusika na tukio hilo.



Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo