Serikali yaomba kusafirisha watuhumiwa wa ‘unga’


Grace Gurisha

SERIKALI imewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiomba kuwasafirisha Ali Hatibu Haji ‘Shikuba’ na wenzake wawili kwenda Marekani kukabiliana na tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Maombi hayo yaliwasilishwa jana kwa nyakati tofauti na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronica Matikila mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha.

Kakolaki alidai kuwa maombi hayo yalianzishwa na Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alipewa nakala ili kufuatilia, ambapo aliwasilisha maombi hayo chini ya sheria ya kusafirisha wahalifu na kuomba yasikilizwe kwa njia ya maneno.

Alidai kuwa maombi hayo ni kwa ajili ya kukamata na kusafirisha kwenda Marekani wajibu maombi hao watatu kwa ajili ya kujibu mashitaka ya kujihusisha na dawa za kulevya.

Alitaja wanaotakiwa kusafirishwa kuwa ni Shikuba, Iddi Mfuru na Tiko Adam. Pia aliomba Mahakama itoe amri ya kuwahifadhi watuhumiwa wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha.

Wakili wa Shikuba, Majura Magafu akishirikiana na Hudson Ndusyepo alieleza kusikia maombi ya upande wa mashitaka na akaomba wapewe muda. Magafu alidai kuwa suala la kumtoa raia wa nchi nje ya nchi si suala rahisi.

Kwa sababu walishafikishwa mbele ya Mahakama aliomba ahirisho ili kupata nafasi ya kupitia makabrasha waliyopewa. Alibainisha kuwa makabrasha hayo ni hati ya ushahidi ambao unatarajiwa kutolewa nje ya nchi.

Hakimu Mkeha aliipanga kesi hiyo ije leo kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo