Hati ya mashitaka ya Ndama kujibiwa leo


Grace Gurisha

Hussein Ndama
UPANDE wa Jamuhuri katika kesi ya kutakatisha fedha chafu inayomkabili mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Hussein Ndama (44), leo unatarajia kujibu hoja za upande wa utetezi kama hati ya mashitaka ina upungufu kisheria au la.

Majibu hayo yanatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya Ndama kulalamika kuwa hati hiyo ina dosari, hivyo kuomba itupiliwe mbali.

Mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro aliomba iahirishwe kwa sababu wakili aliyetakiwa kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi anaumwa.

Upande wa utetezi uliwasilisha hoja kuwa hati ya mashitaka ya mfanyabiashara hiyo ina upungufu wa kisheria, hivyo Mahakama iitupilie mbali hati hiyo na mshitakiwa aachwe huru.

Ndama anakabiliwa na tuhuma sita ikiwamo ya kutakatisha fedha haramu na kujipatia dola 540,390 za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni moja kwa njia ya udanganyifu.

Akitetewa na Wakili Hashimu Rungwe anadaiwa kuwa Februari 20, 2014 akiwa Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya alighushi hati ya kuuza madini nje na sampuli ya madini kwa kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Ltd imemruhusu kusafirisha makasha manne ya dhahabu yenye uzito wa kilo 207 yenye thamani ya dola 8,280,000 zaidi ya Sh bilioni 16 huku akijua si kweli.

Katika tuhuma za pili, mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6, 2014  akiwa Dar es Salaam alighushi hati kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa   Dar es Salaam akionesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilitarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru kwenda kampuni  ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia na kwamba hazina jinai yoyote.

Ilidaiwa kuwa Februari 20, 2014 alighushi nyaraka za malipo zenye namba R. 28092 za Februari 20, 2014 kuonesha kuwa Muru ililipa kodi ya dola 331,200 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya uingizaji kilo 207 za dhahabu zenye thamani ya dola 8,280,000 zilizotoka Congo huku akijua si kweli.

Ndama anashitakiwa pia kuwa, Februari 20, 2014 alighushi bima ya kampuni ya Phoenix of Tanzania Assurance Ltd ya tarehe hiyo ikionesha kuwa Muru iliwekea bima makasha manne ya dhahabu huku akijua si kweli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo