Zitto aishitukia Kenya, ataka mazungumzo


Celina Mathew

Zitto Kabwe
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), ameitaka Serikali kuzungumza na Kenya haraka ili Watanzania wanaouza gesi ya kupikia nchini humo waendelee kutumia bandari ya Dar es Salaam.

Kauli ya Zitto imetokana na hatua ya Wizara ya Nishati ya Kenya, kupiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania ndani ya siku saba.

Zitto alisema tamko lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya lilisema kuwa ndani ya siku saba kuanzia Aprili 24 itakuwa ni marufuku Kenya kuagiza gesi ya kupikia kutoka Tanzania.

“Uamuzi huu wa Kenya ni kinyume na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambamo Tanzania na Kenya ni wanachama. Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa kusambaa ndani ya Jumuiya bila vikwazo,” alisema. 

Alisema gesi ya kupikia kuingia Kenya hutoka nchini, kwa sababu Tanzania ndiyo pekee katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea gesi na kuisindika mitungini katika bandari ya Dar es Salaam na mfumo mzuri zaidi wa kupokea gesi kuliko bandari ya Mombasa, hivyo kuifanya gesi ya nchini kuwa na gharama nafuu Kenya kuliko inayopitia Mombasa.

Aliongeza kuwa uamuzi wa kuzuia gesi ya Tanzania unalenga kulinda bandari ya Mombasa kwa kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutaka kuifanya Tanzania iendelee kuwa muuzaji wa malighafi kwenda Kenya badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani kama gesi ya kupikia. 

“Uamuzi huu wa Serikali ya Kenya una lengo la kuathiri urari wa biashara kati yake na Tanzania ambapo kwa miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa nyingi zaidi Kenya kuliko inazoagiza kutoka nchi hiyo,” alisena na kuongeza:

“Namsihi Waziri wa Biashara na Viwanda nchini afuatilie suala hili na kuzungumza na mwenzake wa Kenya, ili waondoe vikwazo hivi vya biashara ambavyo havina maana yoyote na vinazuia raia wa kenya kupata bidhaa nafuu za Tanzania.”

Zitto alisema viwanda vingi vya Kenya hutegemea malighafi ya Tanzania, hivyo kuzuia gesi hiyo na kuendelea kuagiza malighafi za kuendesha viwanda vyao, ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania chanzo cha malighafi tu na si cha bidhaa zilizoongezwa thamani.

Alisihi Serikali kutokubaliana na hilo na badala yake ifanye mazungumzo mara moja na ya Kenya ili Watanzania wanaouza gesi hiyo Kenya waendelee kuiuza na kutumia bandari ya Dar es Salaam.

“Kama Serikali ya Kenya itaendelea na msimamo wake, basi Tanzania ichukue msimamo kama huo kwa bidhaa za Kenya kama maziwa, ambayo yamejaa kwenye soko letu,” alisisitiza Zitto.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo