Majaliwa aomba viongozi wa dini kueneza uadilifu


Mwandishi Wetu

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mungu, kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya Taifa.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akifungua kongamano kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya, lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dar es Salaam.

Tabia na mwenendo mzuri ni lazima uanzie ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii. Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu itanusurika kwa kiwango kikubwa,” alisema. 

Alisema kila mzazi au mlezi anapaswa kuona aibu, uchungu na kujutia anapoona mtoto akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha, na ni vema wakatumia nafasi yao kuhimiza vijana waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza Mungu.

Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kujenga jamii yenye kuzingatia maadili nchini na kwamba Rais John Magufuli amekuwa akisisitizia Watanzania kuzingatia maadili ya jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na rushwa na ubadhirifu.

Majaliwa alisema maadili kwa Taifa ni moja ya tunu muhimu kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo, ujenzi wa umoja, amani, upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.

“Hivyo hatuna budi nasi kulinda maadili hayo kwa uwezo wetu wote, ili tuyarithishe kwa vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyorithi kutoka kwa waasisi wa Taifa letu,” alisema na kuongeza:

“Hata hivyo, ninyi ni mashahidi kuwa katika siku za karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa maadili na matokeo yake yanaonekana dhahiri, kama kuongezeka kwa rushwa, kuiga utamaduni wa kigeni ambao si mwema na hauna tija kwa jamii, na Taifa kwa ujumla.”

Alisema ni ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo vya matumizi ya dawa za kulevya, hasa kwa vijana na kwamba ni matarajio yake viongozi wa dini wataliangalia kwa kina tatizo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linaathiri Taifa katika mipango yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini yanafanikiwa.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa waathirika wote wa dawa hizo wakiwamo vijana, ambao ni nguvukazi ya Taifa wanakombolewa dhidi ya janga hilo,” alisema.

Alisema Serikali itashughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya  dawa hizo kwa kusimamia sheria ipasavyo.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siyanga aliomba viongozi wa dini kuiunga mkono Mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa inayohitaji msaada wa watu wote.

Mufti wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi alisema viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo