Benki ya Dunia: Uchumi wa Tanzania utakuwa


Suleiman Msuya

BENKI ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi saba za Afrika Kusini mwa Sahara zinazoonyesha ukuaji wa juu wa uchumi kwa mwaka 2015-2017.

Benki hiyo imesema nchi hizo zinazoendelea zimeonyesha ustahimilivu wa kiuchumi, zikisaidiwa na mahitaji ya ndani ambapo viwango vya ukuaji kwa uchumi wake kwa mwaka ni juu ya asilimia 5.4.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia kwenye ripoti yake iliyotolewa jana kupitia Jarida la Africa Pulse, nchi nyingine za ukanda huo zilizo na ukuaji uchumi unaofanana na Tanzania ni Ivory Coast, Ethiopia, Kenya, Mali, Rwanda na Senegal.

“Wakati nchi zikielekea kwenye marekebisho ya sera za fedha, tunahitaji kulinda mazingira sahihi ya uwekezaji ili nchi za Afrika Kusini mwa Sahara ziweze kupata ukuaji imara,” alisema Albert Zeufack, Mchumi Mkuu wa WB Kanda ya Afrika.

Jarida hilo limeenda mbali na kubainisha kuwa uchumi wa nchi hizo unarudi katika kukua kuanzia mwaka 2017, baada anguko baya zaidi kwa zaidi ya miongo miwili liliotokea mwaka 2016.

Ripoti ya jarida hilo ambalo huchapisha uchambuzi wa hali ya uchumi mara mbili kwa mwaka kupitia Benki ya Dunia (WB) ilisema nchi hizo zina takribani asilimia 27 ya idadi yote ya watu wa kanda na zina asilimia 13 ya Pato Ghafi la Taifa la kanda.

Halikadhalika ripoti hiyo imebainisha kuwa mwelekeo wa uchumi wa dunia unaboreka na utaweza kusaidia kurudisha ukuaji katika kanda.

Jarida hilo linaeleza kwamba ukuaji jumla wa bara unatarajiwa kupanda hadi asilimia 3.2 mwaka 2018 na asilimia 3.5 mwaka 2019, ukiakisi uchumi unaorejea kwenye hali ya kawaida katika chumi kubwa zaidi.

Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa ukuaji uchumi utaendelea kuwa mdogo katika nchi zinazouza mafuta nje, wakati nchi zinazouza madini za chuma zinatarajiwa kushuhudia ukuaji wa wastani.

“Ukuaji wa Pato Ghafi la Taifa katika nchi ambazo chumi zake hazitegemei sana madini utaendelea kuwa imara, ukisaidiwa na uwekezaji kwenye miundombinu, sekta za huduma stahimilivu, na kufufuka kwa uzalishaji katika kilimo. Hali hii ni dhahiri kwa nchi za Ethiopia, Senegal, na Tanzania,” ilisema taarifa.

Ripoti hiyo iliweka bayana kuwa kubana zaidi kwa masharti ya fedha duniani kuliko ilivyotarajiwa, maboresho hafifu katika bei za bidhaa na tishio linaloongezeka la sera za kulinda viwanda vya ndani linalotokana na hisia za umma ni hatari zinazoweza kuukumba mwelekeo wa kanda hiyo kiuchumi.

Ilisema kwa upande wa ndani, hatari zinazoweza kuukumba hivyo kurudia ukuaji wa chini wa uchumi ni kasi ndogo ya mageuzi,  kuongezeka kwa vitisho vya usalama na wasiwasi wa kisiasa kabla ya uchaguzi katika baadhi ya nchi.

“Tunahitaji kutekeleza mageuzi ambayo yanaongeza tija ya wafanyakazi wa Kiafrika na kujenga mazingira tulivu ya uchumi mkuu. Kazi bora zaidi na zilizo na tija ni muhimu katika kupambana na umasikini katika bara,” alisema Zeufack.

Alisema mazingira ya ukuaji dhaifu wa uchumi yanakuja wakati bara linahitaji sana kufanya mageuzi ambayo ni muhimu kuinua uwekezaji na kupambana na umasikini.

Mchumi mkuu huyo alisema nchi zinatakiwa kutekeleza maendeleo yanayohitaji fedha nyingi na wakati huo huo kuepuka kuongeza deni la taifa hadi viwango visivyo endelevu.

Alisema katika mazingira hayo, kukuza uwekezaji wa sekta za umma na binafsi, hususani katika miundombinu, ni kipaumbele. “Kanda ilishuhudia mdororo katika ukuaji wa uwekezaji kutoka takribani asilimia 8 mwaka 2014 hadi asilimia 0.6 mwaka 2015,” alisema.

“Wakati viwango vya umasikini vikiwa vingali juu, kufufua kasi ya ukuaji ni muhimu,” anasema Punam Chuhan-Pole, Mchumi Kiongozi wa Benki ya Dunia na mwandishi wa ripoti hii.

Alisema ukuaji unahitaji kujumuisha watu wengi zaidi na utahusisha kukabilina na mdororo katika uwekezaji na gharama za juu za kufanya biashara ambavyo vinazuia uwezo wa kushindana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo