Wahariri wamtaka Lipumba alaani kipigo


Peter Akaro 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemtaka Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alaani kupigwa kwa waandishi wa habari wakati wakitekeleza wajibu wao kwenye mkutano na viongozi wa chama hicho Kinondoni. 

Limesema baada ya tukio hilo la Jumamosi iliyopita, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliandika barua rasmi kwa uongozi wa Jukwaa kulaani kupigwa waandishi hao na kutoa pole kwa walioumizwa na kupata msukosuko. 

TEF ilitoa tamko hilo lenye maazimio sita jana Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, wakiwamo waliopigwa kwenye mkutano huo huku Mwenyekiti wake, Theophil Makunga akibainisha kuwa kupiga na kubughudhi wanahabari hakupaswi kupewa nafasi. 

Tangu tukio hilo, CUF ya Maalim Seif imekuwa ikidai kuwa Profesa Lipumba na kundi lake, ndio waliofanya uvamizi huo, huku wakianika picha za waliohusika kwenye tukio hilo katika mitandao ya kijamii. 

Jumamosi takribani watu watano wakiwa katika gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo kwenye hoteli ya Vinna, Kinondoni na kupiga viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari. 

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso na kofia alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo. 

Katika maelezo yake, Makunga alisema tukio hilo linaingilia uhuru wa habari kinyume cha sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016. 

“TEF itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mikutano ya Profesa Lipumba na wafuasi wake, tusiporidhika na hali ya usalama kwa waandishi wa habari, tutalazimika kuchukua hatua zaidi,” alisema Makunga. 

“Tunatoa mwito kwa wahariri na waandishi wa habari kuchukua hadhari ya hali ya juu wanapoitwa kwenye kundi hili la kisiasa,” alisema Makunga.

Alisema TEF pia ilitoa mwito kwa Polisi kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa uhalifu huo. 

Aliongeza kuwa licha ya mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa fursa ya kuandikwa na kutangazwa habari za pande zote mbili zinazovutana. 

Alisema kitendo cha watu au mtu kushambulia waandishi wa habari walioalikwa kwenye tukio hilo, hakivumiliki na hakikubaliki.

Waandishi waliokumbwa na kipigo ni Fredy Mwanjala (Channel Ten), Asha Bani (Mtanzania), Mary Geoffrey (Nipashe), Mariam Mziwanda (Uhuru), Kalunde Jamal (Mwananchi), Rachel Chizoza (Clouds) na Henry Mwang’onde (The Guardian).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo