ACT yalaani mpinzani kukamatwa Zambia

Suleiman Msuya

Zitto Kabwe
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelaani Serikali ya Zambia kumkamata kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development (UPND), Hakainde Hichilema ‘HH’ kwa madai ya uhaini.

Aidha, chama hicho kimesema vitendo vinavyofanywa na Serikali ya Zambia hasa kwa viongozi wa Upinzani ni ukiukwaji wa misingi ya demokrasia.

Taarifa hiyo ya kulaani ilitolewa jana na Katibu wa Mambo ya Nje wa ACT-Wazalendo, John Mbozu akibainisha kusikitishwa na vitendo vya ukamataji viongozi wa Upinzani katika nchi inayosimamia misingi ya demokrasia.

Alisema vitendo hivyo vinakwamisha juhudi za kukuza demokrasia katika bara la Afrika ambalo linapaswa kukubaliana na mabadiliko ya kidunia.

“Tumelazimika kusema haya kwa sababu matukio ya ukamataji viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani unaonekana kuota mizizi na hii haikubaliki na Tanzania vitendo hivyo vipo pia,” alisema.

Alisema ACT-Wazalendo inaomba wapigania demokrasia, wanaharakati wa haki za binadamu, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) kuzungumzia suala hilo.

Alisema katika kupigania haki za binadamu na heshima ya mtu kokote duniani, chama hicho hakitarudi nyuma ili haki na usawa viweze kupatikana bila kuangalia dini, rangi na mipaka.

“Watu wote tunahitaji heshima na usawa kwa mujibu wa sheria kwa kufanya shughuli bila kuvunja sheria,” alisema.

Alisema Hichilema alishiriki uchaguzi mkuu wa Zambia dhidi ya Rais Edgar Lungu ambapo alimpa wakati mgumu.

Kwa mujibu wa Mbozu, Hichilema alikamatwa juzi usiku nyumbani kwake   New Kasama jijini Lusaka.

Alisema Hichilema atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhaini na kwa mujibu wa sheria za Zambia, akipatikana na hatia atahukumiwa kunyongwa.

Aidha, inasemekana Hichilema hana rekodi yoyote ya makosa ya jinai na kwamba mashitaka hayo ni ya kutengenezwa ili kumaliza ndoto zake za kisiasa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo