Ummy: Wanawake hawatabebwa na sura, umbo


Abraham Ntambara

Ummy Mwalimu
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema hakuna mwanamke atakayebebwa kwa kigezo cha kuwa na umbo wala sura nzuri ili kufikia mafanikio, bali elimu aliyonayo.

Ummy alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipozungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku mbili la kimataifa lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), lenye lengo la kuchunguza kwa kina masuala ya jinsia katika elimu ya juu.

Waziri Ummy aliwataka wanawake kutobweteka na badala yake wajikite kwenye elimu ili kufanikisha malengo ya nchi kwamba hadi mwaka 2025 iwe imefikia 50 kwa 50 katika usawa wa kijinsia.

“Kwa kweli mimi ni mwumini wa elimu kwa wanawake, unaweza ukawa na umbo zuri, unaweza ukawa na sura nzuri, lakini mwisho wa siku tutakuuliza utwambie kiwango chako cha elimu ni kipi, mwanamke habebwi na umbo zuri wala sura, anabebwa na elimu yake,” alisema.

“Nafurahi kusema nami ni mfano bora wa mwanamke ambaye nimetoka katika familia ya kawaida sana pwani, na mnajua watoto wa uswahilini wa pwani hatusomi, mafanikio ya mtoto wa Kiswahili ni kuozeshwa tu,” alisema Ummy.

Alisema kwa sasa nchini hatua kubwa imepigwa katika kuingiza watoto wa kike na wa kiume katika elimu ya msingi na sekondari ambapo alibainisha kuwa imekwishafikia asilimia 50 kwa 50.

Aidha aliipongeza DUCE kwa kufikia asilimia 38 ya watoto wa kike wanaosoma chuoni hapo huku akisema kwa sasa nchi nzima usawa wa kijinsia kwa elimu ya juu ni asilimia 32 kwa wanawake wakati wanaume ni 68.

Alifurahishwa na chuo hicho kufanya kongamano hilo, akisema litasaidia Serikali kuja na mikakati mingine na ya kisasa zaidi ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike kwenye vyuo vya elimu ya juu.

Alifafanua, kwamba kwa kuwa idadi ya wanawake nchini ni zaidi ya asilimia 50, hali ambayo inaonesha kuwa wengi, haitawezekana kuwa na Tanzania ya viwanda endapo watakuwa wameachwa nyuma.

Aliwataka wazazi na walezi kuhamasisha watoto wao kupenda masomo ya Sayansi kwani watoto wa kike wengi hawataki masomo hayo na kueleza kuwa vyuoni vwanaosoma udaktari na uhandisi ni wachache ikilinganishwa na wa kiume.

Mkuu wa DUCE, Profesa William Anangisye alisema kongamano hilo lina nia ya kuleta chachu katika kubainisha nafasi ya wanawake katika maendeleo ya nchi na kuwatia moyo kupenda na kusoma masomo ya Sayansi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo