Mhashamu Eusebius Nzigilwa: Wanaopanga uovu dhidi ya binadamu watashindwa



Mashaka Mgeta
ADHIMISHO la pasaka linalowaunganisha wakristu duniani kukumbuka safari ya mateso, kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristu limefanyika kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Jana ilikuwa Jumatatu ya pasaka ambapo waumini wa dini hiyo na watu wengine wenye mapenzi mema, wanaendelea kuishiriki pasaka hadi itakapofika siku ya pentekoste.

Kwa mataifa yenye Serikali zisizotokana na dini ikiwamo Tanzania, si rahisi sana kuhusisha matukio ya imani na mifumo ya kawaida ya maisha ya watu na shughuli zao hususani siasa.

Lakini undani wa shughuli hizo ikiwamo siasa zinatajwa katika namna inayolenga kuwapo na uongozi bora na mifumo inayochangia watu kuwa na maisha bora ya duniani na mbinguni. Ndivyo ilivyotokea katika pasaka, inavyotokea katika sherehe za Idd el Hajj, Eid al-Fitr, krimasi na nyingine.

Viongozi wa dini wamekuwa wakitumia fursa zinazotokana na sherehe ama maadhimisho hayo
kuwakumbusha watu namna bora ya kuishi na kutenda, ama njia wanazopaswa kuzipita viongozi na watawala katika kuliongoza taifa na watu wake.

Ndio maana viongozi kadhaa wa madhehebu ya Kikristu waliitumia pasaka kuonya, kukaripia, kuelekeza na kufundisha, wakijielekeza zaidi katika matukio ‘yanayoitetemesha’ nchi ikiwamo rushwa, uhasama, ubadhirifu wa mali za umma, vitisho, dhuluma, utekaji, mauaji na uovu mwingine.

Miongoni mwa viongozi hao ni Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa anayeainisha maeneo matatu miongoni mwa mengi yanayopaswa kutafsiriwa kama mafundisho ya pasaka kwa maisha ya watu.

Anayataja maeneo hayo kuwa ni wema dhidi ya uovu ama ukweli dhidi ya uongo, upatanisho na maisha yenye matumaini mapya ya kupata ukombozi. Anapoyataja maeneo hayo, unaweza kupata fikra za mafundisho ya kiroho pekee.

Ingawa ni ukweli usiopingika kuhusu mafundisho hayo kuwa ya kiroho, lakini yanagusa maisha ya watu pasipo kujali tofauti za imani, itikadi ama vinginevyo, isipokuwa pale mhusika (Bwana Yesu) ‘anapotazamwa’ kwa namna tofauti.

Mhashamu Nzigilwa anasema, kwa mfano wa kuundiwa mashtaka, kuteswa na kuuagwa, wakuu wa makuhani waliohofia kwamba kutokana na kazi alizozifanya (Yesu) angeweza kuwaondoa katika madaraka yao. Hawakujua kwamba utawala wake haukuwa wa dunia hii.

Lakini kiongozi huyo wa kiroho anasema hata katika dunia ya sasa, wapo watawala wanaowaundia hujuma watu wema, wakitaka kuwaangamiza ili kukidhi hofu zao na nia ya kulinda kuwapo kwao madarakani.

Ushahidi wa fundishi hilo upo hata katika siasa za nchi nyingi hususani barani Afrika. Viongozi kadhaa wa kisiasa wamekuwa mfano wa waliojimilikisha tawala za kidunia, wakiunda njama na kutumia ushahidi wa uongozi kuwaangamiza wanasiasa na raia wengine wasiokuwa na hatia.

Mhashamu Nzigilwa akasema haipaswi kwa dunia kuwa mahali ambapo mtu asiyekuwa na hatia anaangamizwa ili kulipa maslahi ya watu wengine. “Usipange uovu dhidi ya binadamu hata kipindi cha mpito, utaona umeshinda, lakini elewa kwamba wema hauozi, ukweli utajulikana tu,” anasema.

Fundisho hilo linaweza kuwiana kwa karibu na lile lililowahi kuasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, likaingizwa kwenye ahadi za mwana-TANU, cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

Inapotokea kiongozi akatumia cheo chake ama cha mwingine kwa faida binafsi, ni rahisi kufungua mlango wa kupanga uovu dhidi ya binadamu wengine.

Hivyo Mhashamu Nzigilwa anapolikemea hilo katika sikukuu ya pasaka, anawakemea na wenye dhamana katika ngazi tofauti wanaotumia vibaya madaraka yao dhidi ya wasiokuwa na hatia.

Mhashamu Nzigilwa anasema ipo haja kwa watawala na wenye dhamana kutambua karama tofauti zilizopo kwa watu, kwamba zinapotumika ipasavyo zinachangia katika ujenzi wa taifa.

Kwa upande mwingine, Mhashamu Nzigilwa anasema pasaka inafundisha umuhimu wa upatanisho. Kwamba kama ambavyo Bwana Yesu alirejesha upatanisho kati ya Mungu na wanadamu (kutokana na dhambi ya asili waliyoitenda Adam na Hawa).

Mhashamu Nzigilwa akasema haifai kwa mtu kufurahia mahangaiko ya binadamu mwingine na kwamba kinachopaswa kufanywa ni kumsaidia ili aondokane na kadhia zinazomkabili.

Kwa bahati mbaya `dhambi’ ya kufurahia mahangaiko ya watu imekuwa ikijikita katikati ya watu hata katika siasa, uongozi na utawala. Imekuwa ni kawaida mtu kushangilia hata pale kiongozi ama mtu mwenye dhamana anapotetereka katika kufanya uamuzi ama kutenda inavyostahili, anapoutumikia umma.

Wapo wanaofurahia hata wale wanaopigania haki za watu, wanaposhindwa kufikia malengo yao kutokana na dhuluma na hujuma wanazofanyiwa.

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba upo upungufu usiostahili kuvumilika, unaofanywa na viongozi ama watu wenye dhamana nyingine kwa jamii. Upungufu huo unaweza kuwa katika ukweli halisi lakini unaokosa maana pale ‘inapoongezwa chumvi’ ili kutimiza kusudio la kufurahia mahangaiko ya mtu mwingine.

Kuondoka kwa hali kama hii kunaweza kuwa na faidi nyingi ikiwamo kujenga na kuiimarisha misingi ya umoja na mshikamano wa taifa na ‘kufunga milango’ dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi.

Kwa hiyo taifa linalojijenga katika umoja, linahitaji kuwa na mikakati ya kuwaleta pamoja ikiwamo kupitia njia ya mapatano, ili kwa umoja wao washiriki katika kuilinda nchi, kujiletea maendeleo na ustawi wa kila.

Hatimaye japo si kwa umuhimu, Mhashamu Nzigilwa akataja kuhusu maisha ya matumaini mapya. Akasema kwa asili yake, mtu anapitia njia mbalimbali katika vipindi vyake vya ukuaji. Anahangaika, anakumbwa na shida na wakati mwingine kipindi cha raha. Ni sawa na ilivyo katika majira ya siku kwamba kuna kipindi cha mvua na jua pia.

Inawezekana hali kama hizo zikatokea kwa namna tofauti katika nchi inayopitia awamu tofauti za utawala kama ilivyo Tanzania. Kwamba kulikuwa na awamu ya kwanza (Mwalimu Julius Nyerere), awamu ya pili (Alhaj Ali Hassan Mwinyi) na awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Kisha ikaja awamu ya nne iliyoongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akaikabidhi Ikulu kwa Rais John Magufuli aliyepo katika awamu ya tano.

Katika vipindi ama awamu tofauti, yapo mapito ya magumu ya maisha yanayowakabili watu, kiasi miongoni mwao wanakata tamaa. Mhashamu Nzigilwa anazungumzia maisha ya matumaini mapya.

+255754691540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo