Mvua yakata miundombinu jimboni Chalinze


Mwandishi Wetu, Chalinze

Miundombinu Barabara ya Buyuni
MVUA kubwa iliyoambata na upepo mkali, imekata mawasiliano ya miundombinu ya barabara Buyuni na kusababisha wakazi wa kata za Vigwaza na Mwavi, kupata shida.

Hali hiyo imesababisha wakazi hao kuvushwa kwa kubebwa migongoni kwa ujira wa kati ya Sh 2,000 na Sh 3,000 huku pikipiki zikitoza Sh 5,000 kutokana na  magari kushindwa kupita kabisa.

“Mvua hapa bado haijanyesha, maji haya yanatoka Msoga na kufika huku daraja la Mbiki, Buyuni na kukatiza katika hii barabara, sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu itakuwaje,” alisema Zaina Zuberi aliyekuwa njiani kwenda Mwavi.

Aliongeza: “Barabara ni mbovu kama mnavyojionea, haipitiki, watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani, tatizo ni mkandarasi kwani barabara imejengwa bila makaravati, kila akielekezwa kujenga kutokana na hali halisi ya barabara hafanyi hivyo.”

Baadhi ya vijana wanaosaidia kuvusha watu na pikipiki walisema wabnafanya hivyo kwa makubaliano na wateja wao kwa kuzingatia kipato tangu mvua zianze kunyesha Aprili 7.

“Tunapata fedha kulingana na kichwa cha mtu au pikipiki, kila mtu Sh 3,000 au Sh 2,000 na pikipiki Sh 5,000,“ alisema Rashid Juma.

Aidha, mvua hizo zimeathiri pia barabara ya Milo-Kitonga-Vigwaza.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alitembelea barabara hizo  na kujionea hali halisi.

Ridhiwani alisema hali iliyopo hairidhishi na inawapa wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo na aliahidi kuisimamia kero hiyo kwa kuifikisha bungeni na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili lifanyiwe kazi.

Alieleza kuwa kuna kila sababu ya mkandarasi kufanya kazi kulingana na uhalisia wa eneo husika, hali inayosababisha wananchi kupata tabu na barabara kuharibika kila wakati.

Katika hatua nyingine, Ridhiwani aliunga mkono juhudi za ujenzi wa darasa lililobomoka kwa mvua iliyonyesha Aprili 7 na alichangia   Sh 100,000, mabati 50, mifuko ya saruji 50 na nondo 20.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaya zaidi ya 20 zilikosa makazi na nyumba zaidi ya  90 zilibomoka na nyingine kuezuliwa mapaa jimboni Chalinze, kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali.

Maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ni Chalinze Mzee, Bwawa la umwagiliaji la Msoga ambalo limefumuka na sekondari ya Imperial.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo