Wazee wataka mabadiliko mengine Katiba ya Z’bar


Is-haka Omar, Zanzibar

Dk Shein
BAADHI ya waasisi wa ASP, wasomi na viongozi wa Serikali na kidini jana waliudhuria maadhimisho ya kumbumbuku ya Mashujaa Zanzibar na kuzungumzia umuhimu wa mikakati iliyoachwa na Hayati Mzee Abeid Aman Karume, kuwekwa kisheria ndani ya Katiba ya Zanzibar.

Walieleza kwamba miongozo na fursa za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo ilichoachwa na Mzee Karume inayotekelezwa sasa,  haitoshi kubakia katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Kwa mujibu wa wasomi hao, kuwekwa kwa miongozo hiyo katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kutailazimisha Serikali yoyote itakayoongoza nchi, itekeleze kwa vitendo.

Akizungumza baada ya Dua ya hitima ya maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa ambao ni waasisi wa ASP, waliokomboa Zanzibar toka  utawala wa Kisultani, Waziri  Mkuu  Kassim Majaliwa, alisema Mzee Karume, ameacha urithi wa hazina ya fikra na mawazo ya maendeleo yanayotakiwa kuendelezwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Majaliwa alisema katika miaka nane ya utawala wa Kiongozi huyo, aliwatoa wananchi kwenye giza la uonevu na mateso na kuwaweka kwenye mwanga wa mafanikio ya kimaendeleo, yanayoendelezwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed akitoa nasaha zake kwa wananchi, aliwasihi kuendelea kuunga mkono Serikali iliyopo madarakani kwani ndiyo inayosimamia na kutekeleza, fursa zilizoachwa na waasisi wa ASP waliowekewa siku maalum ya kitaifa kukumbukwa kwa kusomewa dua kutokana na juhudi zao za kukomboa nchi.

Alisema Zanzibar itaendelea kuimarika kiuchumi endapo kila mwananchi bila ya kujali itikadi za kisiasa na kidini, atalinda amani, utulivu na kuchukia kwa vitendo ubaguzi, kama ilivyokuwa kwa mashujaa wa ASP walivyoondosha utawala wa mabavu.

“Leo tumeadhimisha kumbukumbu ya mashujaa wetu lakini bado tuna kazi kubwa ya kulinda na kuendeleza urithi wa wazee wetu, kwani bado zipo choko choko za baadhi ya watu wenye nia ya kuchafua amani ya nchi yetu, lakini na sisi wajue tupo imara kama wazee wetu walivyokuwa mashujaa na kutetea maslahi ya wanyonge,” alielea Waziri Aboud.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wakulima (AFP) Zanzibar, Said Soud  Said amesema kazi aliyofanya Mzee Karume ndio iliyozaa matunda ya Wazanzibari kuishi kwa utulivu na kujiamulia mambo yao wenyewe.

Alisema ukombozi wa Zanzibar wa mwaka 1964 aliousimamia yeye ndio hasa kioo cha Wazanzibari duani nzima kujiona kuwa wapo huru na wenye uwezo wa kujenga Taifa lao kiuchumi bila vikwazo vyovyote.

Soud ambaye pia ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum  wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema baada ya mapinduzi hayo Mzee Karume aliweka misingi iliyofuatwa na viongozi waliotawala baada yake ambayo kwa sasa wananchi wote wa Zanzibar wananufaika nayo.

Asha Simba Makwega aliyelelewa na Mzee Karume na baadae akawa kada wa ASP, alisema kiongozi huyo alitumia muda wake kushughulikia kero na matatizo ya wananchi, kuliko muda alioutumia kwa familia yake, hali inayothibitisha uzalendo na utaifa wa kweli wa shujaa huyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo