Miaka 2 jela kwa wizi wa milioni 2/-


Jemah Makamba

MKAZI wa Buguruni Dar es Salaam, Fatuma Yusufu (40) amehukumiwa kwenda jela miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh milioni mbili mali ya Natoza Haule.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Benjamin Mwakasonda wa Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo, alisema Mahakama ilijiridhisha na ushahidi dhidi ya mlalamikiwa na kumtia hatiani.

Hakimu alisema ushahidi uliotolewa na mlalamikaji ambaye ndiye alikuwa shahidi namba moja katika kesi hiyo, ulithibitisha namna alivyoiba fedha hizo.

Awali shahidi alidai mahakamani hapo kwamba siku ya tukio, akiwa mfanyakazi wa usafi katika Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam, alifika wa kwanza asubuhi na kumwomba mlinzi ufunguo ili aanze usafi.

Alidai kuwa baada ya kufika ofisini mwake alikuta droo yake imevunjwa na fedha alizokuwa ameacha zimetoweka.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya hapo alimtafuta mlinzi na kumhoji nani alikuwa wa kwanza kuingia akaambiwa ni mtu wa usafi ambaye ni mshitakiwa na alikuwa ameondoka eneo hilo na hakutokea hadi alipokamatwa.

Kutokana na ushahidi huo, mshitakiwa alikutwa na kesi ya kujibu na Mahakama kumtia hatiani kwa wizi.

Hakimu alimwuliza Karani, Saidi Benea kama kuna kumbukukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa akasema hakuna ila mshitakiwa apewe adhabu kali iwe fundisho.

Mshtakiwa aliulizwa na Hakimu kama kuna chochote cha kuiambia Mahakama kabla ya kupewa adhabu.

"Hakimu mimi ni mgonjwa, naumwa na natumia dozi lakini pia mama yangu mzazi ni mzee sana, mimi ndiye namtunza naomba huruma yako," mshitakiwa aliomba.

Maombi hayo hayakumzuia Hakimu kutoa adhabu hiyo, ya kwenda jela miezi 24 na akitoka alipe fedha hizo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo