TFDA: Mafuta ya alizeti ni salama


Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imewataka wananchi kuendelea kutumia mafuta ya alizeti yaliyothibitishwa nayo.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa TFDA, ilisema imefanya uchambuzi wa awali wa matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2014/15 na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhusu mafuta hayo.

Ilisema utafiti huo ulihusu mbegu za alizeti na mashudu kuchafuliwa na sumukuvu aina ya Aflatoxins, hivyo vyombo vya habari juzi kutoa hadhari kwa watumiaji.

“TFDA imefanya uchambuzi wa awali wa matokeo ya utafiti huo na kubaini kwamba ulihusu mbegu za alizeti na mashudu pakee na hivyo hautoshelezi kuthibitisha kuwa mafuta ya alizeti yamechafuliwa na Aflatoxins kwa kiwango ambacho ni hatarishi,” ilisema taarifa.

Hata hivyo, TFDA ilisema itafanya uchambuzi wa kina wa matokeo ya utafiti yaliyochapishwa kwenye jarida la PLOS One na kufanya ufuatiliaji na uchunguzi zaidi wa mbegu, mashudu na mafuta ya alizeti yaliyozalishwa nchini.

“Mwito unatolewa kwa watafiti nchini wanaofanya utafiti kuhusu usalama na ubora wa chakula, dawa, vipodozi, vifaatiba na vitendanishi, kushirikisha TFDA kama mdau muhimu juu ya matokeo ya utafiti wao ili yatumike kuimarisha mifumo ya udhibiti na hivyo kulinda afya ya jamii,” ilifafanua taarifa hiyo.

Vyombo vya habari vilishauriwa pia kuwasiliana na TFDA kupata maoni na tafsiri sahihi kuhusu matokeo ya utafiti wa kisayansi kuhusu usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaatiba na vitendanishi, kabla ya kuchapisha ili kuondoa uwezekano wa kuleta hofu kwa jamii.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo